Saturday 27 June 2015

Chadema yaibwaga CCM kesi za uchaguzi

]

MAHAKAMA ya Wilaya ya Igunga mkoani Tabora juzi ilitupilia mbali kesi tano zilizokuwa zimefunguliwa na Chama Cha Mapinduzi (CCM) dhidi  ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema)  katika uchaguzi wa Serikali za Mitaa uliofanyika  Desemba 14, mwaka jana.

Kesi hizo zilifunguliwa na CCM katika Mahakama ya Wilaya ya Igunga Aprili, mwaka huu, ambapo chama hicho kilikuwa kikipinga ushindi walioupata wenyeviti watano wa Serikali za Mtaa, ukiwemo wa Stoo, Kamando, Mwayunge, Nkokoto na Kijiji cha Simbo wilayani humo.

Akisoma hukumu hiyo, Hakimu wa Mahakama ya Wilaya ya Igunga,  Leonadi Nkola, alisema madai yalitengenezwa na mtayarishaji  mmoja, hivyo kila neno na sentesi zilifanana na tofauti yake ni katika majina na katika makosa yaliyofanywa baada ya uchaguzi, mawakala wao waliweza kusaini na kukubaliana na matokeo kwa msimamizi mkuu wa Uchaguzi wa Wilaya na kwenda kinyume cha sheria.

Aidha Hakimu Nkolo alibainisha kuwa katika madai yao pia hawakuweza kuonyesha barua yoyote ambayo walimwandikia msimamizi wa uchaguzi wa wilaya inayopinga matokeo ya ushindi.

Akiendelea kusoma hukumu hiyo, Nkola alisema katika hati hiyo ya madai iliyoandaliwa haikuweza kutoa nukuu ya kifungu cha sheria kinachothibitisha ukiukwaji wa uchaguzi huru na haki kwa kuvunja sheria na kanuni za uchaguzi na kufanya madai yao kutokuwa ya msingi na sheria.

Kutokana  na kukosekana uthibitisho wa madai hayo, Mahakama ilitupilia mbali madai hayo na kusema kuwa hao ni viongozi haramu wa Serikali za Mitaa.

Viongozi wa CCM walioshindwa ni pamoja na Julius Mpuya Mtaa wa Kamando, Abeid Issa wa Mtaa wa Nkokoto, Majenga Mashauri Mtaa wa Stoo, Ally Isike Mtaa wa Mwayunge na Athuman Mohamed wa Kijiji cha Simbo,

Aidha viongozi walioshinda upande wa Chadema ni Joseph Njile wa Mtaa wa Stoo, Abel Shampinga Mtaa wa Mwayunge, Gerad Ndezi Mtaa wa Nkokoto, Julius Kitundu Mtaa wa Kamando na Yusuph Finyongolo  wa Kijiji cha Simbo.

No comments: