Monday 20 July 2015

Benard Membe Atangaza Kuachana Na Siasa.......Asema Hatagombea Wadhifa Wowote Mwaka Huu


Waziri wa Mambo ya Nje na  ushirikiano wa kimataifa, Bernard Membe, amesema hatogombea wadhifa wowote kwenye uchaguzi mkuu wa  mwaka huu na kwamba anapanga kujishughulisha na masuala yake ya kibinafsi.

Membe ambaye alikuwa akitafuta tiketi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) ili kuwania urais mwezi Oktoba lakini akashindwa kufikia lengo hilo, amesema kuwa, hatotafuta nafasi ya ubunge katika jimbo lake la Mtama.

Hata hivyo amesema ataendelea kukiunga mkono chama chake cha CCM na atampigia debe mgombea urais aliyeteuliwa na chama hicho, Bw. John Magufuli.

Awali kulikuwa na tetesi kwamba Membe angegombea ubunge baada ya kukosa nafasi ya kuwania urais kwa tiketi ya CCM.

Huku hayo yakijiri, chama cha Mapinduzi  (CCM) kinaendelea kupata pigo baada ya baadhi ya wabunge wake kutangaza kuwa hawatogombea tena nafasi zao kupitia chama hicho kwenye uchaguzi mkuu ujao.

Tayari madiwani 20 wa CCM katika jimbo la Monduli wametangaza kuhamia Chadema na kumtaka mbunge wao, Edward Lowassa kufuata mkondo huo.

No comments: