Monday 20 July 2015

Mbunge wa Viti Maalumu kwa tiketi ya CCM, Ester Bulaya Amekataa Kuchukua Fomu ya Ubunge kwa tiketi ya CCM.


Hali imeendelea kuwa tete ndani ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), baada ya aliyekuwa Mbunge  wa Viti Maalum CCM mkoa wa Mara, Ester Bulaya, kutangaza kukitosa kwa kutangaza uamuzi wake wa kutogombea ubunge kwa tiketi ya chama hicho.


Bulaya ambaye alikuwa mbunge machachari kabla ya Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kuvunjwa na Rais Jakaya Kikwete, hivi karibuni , ametangaza kutogombea ubunge kupitia CCM wakati akizungumza na mtandao huu  baada ya kazi ya kuchukua fomu ndani ya chama hicho na kurejesha kuhitimishwa rasmi nchini jana.

Tangu mwanzo mwa mwaka huu, Bulaya alitangaza kugombea ubunge katika Jimbo la Bunda kupambana na Mbunge aliyemaliza muda wake ambaye ni Waziri wa Kilimo, Chakula na Ushirika, Stephen Wasira.

Bulaya amekuwa kada wa pili ambaye alikuwa mbunge kutangaza kutogombea ubunge kwa tiketi ya CCM, mbunge wa kwanza kutangaza kutogombea ubunge  kupitia CCM baada ya James Lembeli, ambaye alikuwa Mbunge wa Kahama.

Hata hivyo, Bulaya hakuweka wazi kama ana mpango wa kuhamia chama kingine cha siasa na kutimiza azma yake ya kuwania ubunge katika uchaguzi mkuu wa mwaka huu.

Ingawa Bulaya hajaweka wazi, vyama ambavyo vimekuwa vikitajwa kusubiri makada kutoka CCM kujiunga navyo ili wawanie ubunge ni Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), ACT-Wazalendo na Chama cha Wananchi (Cuf).

Mwenyekiti Monduli Apigilia Msumari
Wakati ikiwa hivyo kwa Bulaya, hali bado si shwari ndani ya CCM Wilaya ya Monduli baada ya aliyekuwa Mwenyekiti wa Halmashauri ya Monduli, Edward Sapunyo, Kupigilia msumari wa mwisho na kubariki hatua ya madiwani wake 20 kukihama chama hicho na kujiunga na Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema).

Akizungumza mjini hapa jana, Sapunyo ambaye alikuwa Diwani wa kata ya Moita, alisema madiwani wake hawawezi kusubiri hadi Mbunge wa Jimbo la Monduli na Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa, atoe kauli kuhusu hatma yake ya kisiasa ndani ya CCM.

Kauli ya Sapunyo ambaye hatagombea udiwani uchaguzi wa mwaka huu, imekuja siku moja baada ya madiwani 20 wa jimbo hilo kutangaza rasmi kukihama chama hicho na kujiunga na Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema).

“Hatuwezi kuona baba yetu anapigwa na kuanguka chini halafu tusubiri kauli yake, ni lazima tuchukue hatua mara moja…hii haivumiliki, kitendo alichofanyiwa (Lowassa) na vikao vya CCM mjini Dodoma hivi karibuni kwa kukata jina lake pasipo kumpa haki ya kumsikiliza siyo cha kidemokrasia,” alisema.

Lowassa na makada wenzake wa CCM 38 walichukua fomu ya kuomba  ridhaa ya kuteuliwa na chama hicho kupeperusha bendera ya kuwania kiti cha urais katika uchaguzi mkuu unaotarajiwa kufanyika Oktoba 25, mwaka huu.

Katika kinyanyang’anyiro hicho, jina la Lowassa na wenzake yalikatwa katika hatua ya mwanzo, hali ambayo imezua malalamiko kwamba ikidaiwa kuwa hawakupewa
nafasi ya kuhojiwa.

“Tumepigwa, tumesambaratika (CCM) Monduli, hatuwezi kuchukua fomu za kuomba kugombea au kutetea nafasi zetu ndani ya chama hiki, tumehamia Chadema,” alisema.

Akizungumzia hali ilivyo, Katibu wa CCM Wilaya ya Monduli, Elisante Kimaro, alidai kuwa siyo kweli kwamba madiwani wote wamekihama chama chao.

Kimaro alidai kuwa baadhi ya madiwani waliotangaza kukihama chama hicho wameanza kusalitiana.

Alisema madiwani hao ambao anawaita ni makada baada ya Baraza la Madiwani la Halmashauri ya Monduli kuvunjwa, walifanya mkutano kwa kushawishiwa na mmoja wao.

Alisema ushawishi huo unatokana na uchu wa madaraka alionao kwa kuwa tayari wananchi wa Jimbo la Monduli, wanapenda aliyekuwa Mbunge wa Viti Maalum CCM, Namelok Sokoine, kuchukua fomu za ubunge wa jimbo hilo.

Alisema kutokana na ugumu huo, diwani huyo wa zamani ametumia mbinu ya kuwarubuni wenzake wakihame chama hicho ili agombea ubunge kwa tiketi ya Chadema.

“Huo ni uchu wa madaraka aliyo nayo,” alisema na kuongeza: “Diwani huyo hakubaliki na wananchi wa kata yake."

Alidai kabla ya kutangaza kukihakama chama hicho, madiwani hao walikuwa wameshafanya kikao na kuweka azimio la pamoja la kuondoka CCM, lakini juzi walipotangaza uamuzi wao, walijikuta wapo madiwani watatu.

Alisema baadhi ya madiwani walimfuata ofisini kwa lengo la kumuomba radhi lakini yeye aliwaambia waende kuwaomba radhi wananchi katika kata zao.

“Madiwani wachache walikuja hapa ofisini kuomba radhi kwa Katibu wa CCM Wilaya, nikawaambia waende kuwaomba radhi wananchi,” alisema.

Akimzungumzia Lowassa, alisema anachoelewa ni kwamba hajatoa tamko lolote kama anakihama chama hicho kama inavyodaiwa na baadhi ya watu na mitandao ya kijamii.

“Bado tuna imani na Lowassa kuwa ni CCM, mpaka sasa hajatoa tamko lolote kukihama chama, lakini ikiwa vinginevyo itakuwa hatari kubwa,” alisema.

No comments: