Sunday 31 January 2016

Serikali Yakataa Maombi Yote Ya Shule Binafsi Kupandisha Ada Mwaka Huu

Kamishna wa Elimu nchini amekataa maombi yote ya shule za msingi na sekondari zisizo za Serikali kupandisha ada katika mwaka huu wa masomo na ameagiza shule zilizopandisha ada kinyume cha tamko la Serikali kusitisha ada hizo mpya.

Kutokana na uamuzi huo, Wizara ya Elimu, Sayansi, Teknolojia na Ufundi imeziagiza shule zote za binafsi ambazo zimepandishia ada kiholela bila kupata kibali cha wizara hiyo, kurejesha ada waliyokuwa wanatoza mwaka jana, la sivyo hatua kali zitachukuliwa kwa shule itakayokaidi.

Kaimu Mkurugenzi Idara ya Ithibati ya Shule, Hadija Mcheka amesema baada ya tangazo la wizara hiyo kuzitaka shule binafsi zinazotaka kupandisha ada kuwasilisha maombi kwa Kamishna wa Elimu na kutoa sababu za kupandisha ada, ni shule 45 tu zilipeleka maombi ya kupandisha ada wakati shule zingine 900 ziliomba ziendelee kutoza ada ya mwaka jana.

“Hizi shule 45 hazikupata kibali cha kupandisha ada maana sababu walizozitoa hazikumridhisha Kamishna wa Elimu hivyo akaamuru zibakie na ada ya mwaka jana,” alisema Mcheka. 

Tanzania ina jumla ya shule za msingi 14,000 na kati ya hizo shule binafsi ni 1,000.

Kwa upande wa sekondari, shule binafsi ziko zaidi ya 1,400 kati ya sekondari 4,000. Mcheka alifafanua kuwa baadhi ya shule zilitoa sababu kuwa wanapandisha ada kwa sababu wana ujenzi, jambo ambalo kamishna aliona halimhusu mzazi.

“Mwingine anasema anataka kupandisha ada kwa vile anataka kuajiri walimu kutoka nje ya nchi, hili nalo halimhusu mzazi ndio maana tumewanyima kibali cha kupandisha ada,” alieleza.

Pia alisema shule zingine zilinyimwa ruhusa ya kupandisha ada kwa sababu hazikutoa sababu yoyote zaidi ya kueleza kuwa wanataka kupandisha ada kutokana na gharama za uendeshaji.

“Sababu zote hizi hazikumridhisha kamishna ndio maana tumewataka watii agizo la Serikali hadi hapo baadaye.” Alifafanua. 

Mcheka alisema hatua ya kuzitaka shule zote zibaki na ada ya mwaka jana ni kutokana na wizara hiyo kumwajiri mtaalamu mwelekezi anayefanya kazi ya kujua gharama za kumsomesha kila mwanafunzi ili kuisaidia Serikali kuweka ada elekezi.

Alisema ada elekezi hiyo ndio itakayoisaidia wizara kupanga ada elekezi kwa shule binafsi. 

Aliwaonya wamiliki wa shule binafsi ambao wamepuuza agizo hilo kwa kisingizio kuwa hawajapelekewa barua na wizara husika kwamba watachukuliwa hatua kali za kisheria zilizoainishwa wakati shule inaposajiliwa.

Alisema Serikali inafanya kazi kupitia waraka, matamko na maagizo ambayo lazima wahusika wanaohusika kuyatiii na sio kusubiri kuandikiwa barua. 

“Katika hili hatutanii kama zipo shule ambazo hazikutii tamko lile la Serikali na wakapandisha ada naomba wasitishe ada hizo mpya,” alionya.

Mcheka aliwataka wazazi na walezi walioanza kulipa ada hiyo mpya kusitisha malipo hayo mara moja na kwamba wahakikishe kuwa ada yote watakayolipa kwa mwaka huu ifanane na ile iliyolipwa mwaka jana na sio vinginevyo.

“Kama mwaka jana alilipa Sh milioni 1.5 na mwaka huu amepandishiwa hadi Sh milioni 1.8, na kwa kuwa mzazi analipa kwa term (muhula)na tayari ameshalipa term ya kwanza, naomba atakapolipa muhula wa pili alipe pesa pungufu ya kile alicholipa term (muhula) ya kwanza ili zitimie Sh milioni 1.5 na sio Sh milioni 1.8,”alisema Mcheka.

Aliwataka wazazi na walezi kutoa taarifa wizarani na ofisi za elimu za wilaya kwa shule ambazo zitakaidi agizo hilo ili hatua ziweze kuchukuliwa. 

No comments: