Tuesday 11 October 2016

A tuhumiwa kuzika maiti ya mwanaye chumbani kwake

Na Gordon Kalulunga, Mbeya

Mwananchi aliyetajwa kwa jina la Shadrack Simbeye mkazi wa Kitongoji cha Tunduma Road Mapelele mjini Mbalizi, wilaya ya Mbeya mkoani hapa, amezika maiti ya mwanaye chumbani kwake.
 
Hali hiyo imeleta sintofahamu kwa wakazi wa eneo hilo na kuhusisha tukio hilo na masuala ya kishirikina.

Tukio hilo limegundulika leo baada ya Shadrack Simbeye jana kutoa taarifa ya msiba wa mtoto wake mchanga ambaye alifariki mara baada tu ya mkewe aliyefahamika kwa jina maarufu la mama Baraka kujifungua katika Hospitali ya Rufaa ya Mbeya kitengo cha wazazi Meta na mtoto kufariki.

Akizungumza na mwandishi wa habari hii, Mwenyekiti wa Kitongoji cha Tunduma Road Bw. Bahati Nyalile, amethibitisha kuwepo kwa tukio hilo.

Amesema jana mfiwa alienda kutoa taarifa ya kifo cha mtoto wake na kuomba kumzika nyumbani kwake.

"Tulimwambia hapa hatuna utaratibu wa kuzika majumbani bali utaratibu ni kuzika katika makaburi ya jumuiya, alikubari na kwenda kuchimba kaburi lakini baadae tukaambiwa kuwa hakupeleka maiti" alisema Nyalile.

Alisema masikitiko yake ni kwa Jeshi la Polisi ambao baada ya kupata taarifa walifika eneo la tukio na kuogopa kuingia ndani huku wakikataa hata kujiridhisha mbele ya viongozi wa eneo husika.

"Siku nyingine kwa upande wangu sintoweza kutoa taarifa Polisi, maana wao wanaonekana kujua kukamata wananchi wanaojitafutia riziki kuchimba mchanga mtoni na hii ni ishara ya Polisi kuruhusu maziko majumbani" alisema huku akisema atafikisha taarifa kwa Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mbeya.

Diwani wa kata hiyo ya Nsalala, Kissman Mwangomale, amesema alipopata taarifa ya tukio hilo alimtaarifu Mkuu wa kituo cha Mbalizi na Ofisa Mtendaji wa Mamlaka ya mji mdogo wa Mbalizi.

"Ni tukio baya na la kushangaza, tunasubiri mamlaka za serikali hatua watakazochukua" alisema Mwangomale.

Kwa upande wake Ofisa mtendaji wa Mamlaka ya mji wa Mbalizi Bw. Kassim Ugulumo alipotafutwa kwa njia ya simu hakuweza kupokea.

Ofisa Mtendaji wa kata hiyo Joseph Stimar, amesema yeye hajafanikiwa kufika eneo la tukio kwasababu ya majukumu mengine ya kikazi, lakini amekiri kupata taarifa za tukio hilo.

"Nimepata taarifa za tukio hilo na kwamba kule makaburini alienda kuzika tofali, lakini naendelea kufuatilia" amesema Stimar.

No comments: