
Mtu ambaye hajafahamika akimtishia bastola aliyekuwa Waziri wa Habari,
Utamaduni, Sanaa na Michezo, Nape Nnauye alipotaka kuzungumza na
waandishi wa habari jijini Dar es Salaam. Picha na Maktaba
Mtwara: Inspekta Jenerali wa Polisi, Simon Sirro amewataka wananchi wenye taarifa kuhusu alipo mtu aliyemtolea bastola hadharani Mbunge wa Mtama, Nape Nnauye wafanye hivyo.
IGP Sirro leo Jumatano akiwa ziarani mkoani Mtwara amesema mtu huyo alikimbia na Jeshi la Polisi linaendelea kumtafuta.
Amesema kuonekana kwa picha za mtu huyo haina maana kwamba atapatikana kwa urahisi hivyo jeshi hilo linaendelea kumtafuta.
“Mheshimiwa
Nape amefungua kesi. Ujue picha kuonekana haina maana kwamba yule mtu
ataonekana kirahisi lakini upelelezi unaendelea kumtafuta aliyefanya
tukio hilo. Wananchi watusaidie, maana suala la kumpata mhalifu ni
ushirikiano, sisi tunaenda kwa taarifa, bila taarifa ya uhakika hatuwezi
kufanikiwa,” amesema.
Akizungumzia uhalifu wilayani
Kibiti, IGP Sirro amesema baadhi ya watuhumiwa wamekimbilia mkoani
Mtwara na wataendelea kuwashughulikia.
Amewataka
wanaojihusisha na uhalifu yakiwemo mauaji ya raia kuacha vitendo hivyo
alivyoviita vya hovyo. Amesema kukimbia hakuwasaidii badala yake waache
na kuwa raia wema.
“Kuna changamoto, waliokuwa Kibiti
nasikia baadhi yao wamekimbilia huku na bahati nzuri tuna vijana wetu
pia wameingia hapa,” amesema.
IGP Sirro amesema,
“Niliwaambia hakuna salama yao katika Tanzania labda wakimbilie sehemu
nyingine, lakini Mtwara bado iko Tanzania na ukienda Lindi bado iko
Tanzania, tutawapata huko waliko na tutawagonga vizuri kwa mujibu wa
sheria kwa sababu wao ndio wameanzisha ligi. Ukianzisha ligi jitahidi
kumaliza ligi sasa kumaliza ligi si kukimbilia Mtwara.”
No comments:
Post a Comment