Kamanda wa Kikosi cha Usalama Barabarani, Fortunatus Muslim amepiga marufuku tabia ya baadhi ya madereva nchini kubeba abiria kwenye magari ya mizigo ili kuepusha madhara makubwa pindi ajali zinapotokea barabarani.
Kamanda Fortunatus Muslim amepiga marufuku hiyo leo wakati akiongea na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam na kutoa masikitiko yake kufuatia vifo vya watu 15 waliofariki kwenye ajali ya gari aina ya Fuso lililokuwa likitokea Sumbawanga mjini na kwenda Wampembe mwambao mwa ziwa Tanganyika wilayani Nkasi mkoani Rukwa baada ya gari hilo kupinduka katika eneo la Ntembwa mkoani Rukwa.
Kwa mujibu wa Kamanda Muslim anadai Lori hilo mali ya Bwana Bakari Kessy lilikuwa limebeba shehena ya viroba vya mahindi na abiria hivyo gari lilipinduka katika pori la akiba la Lwafi mwambao mwa ziwa Tanganyika baada ya kumshinda dereva katika kona kutokana na mwendokasi.
Kamanda Muslim ameahidi kuwachukulia hatua kali za sheria madereva wote ambao watakiuka agizo hilo lililotolewa leo Oktoba 4, 2017.
No comments:
Post a Comment