VODACOM yatoa tamko kuhusu Udhamini wake Ligi Kuu Bara!
Jumatano, 26 Septemba 2012 14:46
>>TFF yatoa Taarifa!!
ZIFUATAZO ni TAARIFA KUTOKA VODACOM na TFF:
TAARIFA KUTOKA VODACOM:
Taarifa kwa vyombo vya habari.
Vodacom yazungumzia kipengele cha Upekee (Exclusivity) katika mkataba wa udhamini wa Ligi Kuu.
Dar es salaam 25th September 25, 2012, Kampuni ya Mawasiliano ya Vodacom Tanzania imesema suala la kuwepo kwa kipengele cha Upekee “EXCLUSIVITY”
katika mkataba wa udhamini wa ligi kuu soka Tanzania bara kati ya
kampuni hiyo na shirikisho la soka nchini - TFF ni la muhimu katika
kuepuka migongano ya kimasilahi ya kibiashara miongoni mwa wadhamini.
Mkuu wa Udhamini na Mawasiliano wa
kampuni ya Vodacom Tanzania Bw Kelvin Twissa amesema kampuni ya Vodacom
inajali na kuthamini maendeleo ya vilabu nchini na kwamba itaendelea
kufanya hivyo kwa kutoa fursa zaidi zinazolenga kukuza kiwango cha
uwekezaji katika soka kwa masilahi ya vilabu na taifa kwa ujumla.
Twissa amesema katika kutambua umuhimu
wa kupanua wigo wa uwekezazi katika ligi kuu ya Vodacom na maendeleo ya
vilabu kwa ujumla, kampuni ya Vodacom Tanzania ilikubali kwa moyo
mkunjufu kuruhusu vilabu kutafuta wadhamini wengine ambao siyo makampuni
yanayofanya baishara sawa na Vodacom.
Twissa alikuwa akizungumza katika kikao
cha pamoja kilichowakutanisha Shirikisho la Soka Tanzania – TFF, Kamati
ya Ligi Kuu na Mdhamini Mkuu kampuni ya Vodacom Tanzania kilichoketi
jana jijini Dar es salaam.
“Tunatambua na kuheshimu utayari wa
makampuni mengine ambayo yapo tayari kushirikiana na sisi katika
kudhamini Ligi kuu ya Vodacom nasi tupo tayari kushirikiana nao na hivyo
kuleta maendeleo ya mpira wa miguu nchini”Alisema Twissa
“Vodacom Tanzania inajivunia kuwa
wadhamini wakuu wa ligi hii,tumeamua kuboresha udhamini wetu kwa sababu
tunatambua umuhimu wa michezo kwa Taifa letu, sasa michezo si kwa ajili
ya burudani tu bali imekuwa chanzo cha ajira na kuboresha maisha ya
wanaojihusisha nayo,” Aliongeza Twissa.
“Tunaviomba vilabu vinavyoshiriki ligi
kuu, vyombo vya habari na umma kwa ujumla kutambua kuwa azma ya Vodacom
ni kuona mpira wa miguu unasonga mbele zaidi na ndio maana tumekuwa
katika udhamni huu kwa zaidi ya miaka saba tukipitia vipindi tofauti
lakini hatukuwahi kukata tamaa. Hivyo si vyema wakati huu soka yetu
inapokua tukaruhusu hali inayoweza kusababisha changamoto katika
uwekezaji wa soka.” Aliongeza Twisa
Twissa amesema kampuni ya Vodacom
itaendelea kushirikiana na TFF, Kamati ya Ligi na wadau wengine wote wa
mpira wa miguu nchini katika kukuza uwekezaji kwa kusaidia vilabu kupata
wadhamini watakaosaidia maendeleo ya vilabu hivyo.
Mwisho
TAARIFA TOKA TFF:
Release No. 155
TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
Septemba 26, 2012
KAMATI YA UCHAGUZI TFF YATUPA RUFANI YA WARUFANI IRFA
Kamati ya Uchaguzi ya Shirikisho la
Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) ilikutana jana (Septemba 25 mwaka huu)
kusikiliza rufani iliyowasilishwa mbele yake na warufani Mussa H.
Mahundi, Abou O. Sillia na Alex Mgongolwa dhidi ya Kamati ya Uchaguzi ya
Chama cha Mpira wa Miguu Mkoa wa Iringa (IRFA) iliyoomba Kamati ya
Uchaguzi ya TFF kubatilisha matokeo ya uchaguzi wa IRFA uliofanyika
Septemba 8 mwaka huu Mufindi, Iringa, na kuomba uchaguzi huo ufanyike
upya kwa kuendeshwa na kusimamiwa na Kamati ya Uchaguzi ya TFF.
Kwa mujibu wa Mwenyekiti wa Kamati ya
Uchaguzi ya TFF, Deogratias Lyatto, baada ya kupitia maelezo ya warufani
na warufaniwa, Kamati ya Uchaguzi ya TFF imejiridhisha kuwa rufani
iliyowasilishwa mbele yake na Mahundi, Sillia na Mgongolwa ilikosa sifa
ya kuwa rufani kwa mujibu wa Kanuni za Uchaguzi za Wanachama wa TFF,
Ibara ya 8(2), Ibara ya 21(3) na 24(2). Kwa kutozingatia matakwa ya
Kanuni za Uchaguzi za Wanachama wa TFF, Kamati ya Uchaguzi ya TFF
imetupa rufani hiyo.
Kamati ya Uchaguzi ya TFF imeiagiza
Kamati ya Uchaguzi ya IRFA kuchukua hatua dhidi ya Abuu Changawa kama
ilivyoainishwa kwenye Kanuni za Uchaguzi za Wanachama wa TFF, Ibara ya
28(6) kwa kuingilia mchakato wa uchaguzi wa IRFA siku ya uchaguzi.
SHUKRANI KWA WADAU SERENGETI BOYS
Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania
(TFF) linawashukuru wadau waliofanikisha kwa njia mbalimbali ziara ya
timu ya Taifa ya vijana wenye umri chini ya miaka 17 (Serengeti Boys)
iliyofanyika hivi karibuni katika mikoa ya Mbeya na Njombe.
Wadau hao ni Chama cha Mpira wa Miguu
Mbeya Mjini (MUFA) chini ya Mwenyekiti wake Suleiman Haroub, Kaimu
Mwenyekiti wa Chama cha Mpira wa Miguu Mkoa wa Njombe (NJOREFA), Stanley
Lugenge, Chama cha Mpira wa Miguu Mkoa wa Mbeya (MREFA) na Chama cha
Mpira wa Miguu Wilaya ya Njombe (NDFA).
Wengine ni Chama cha Mpira wa Miguu
Wilaya ya Makambako (MDFA), Chama cha Mpira wa Miguu Mkoa wa Morogoro
(MRFA), na klabu za Mbozi United, Kyela United, Tanzania Prisons na
Mbeya City.
Serengeti Boys inaendelea na kambi yake
jijini Dar es Salaam kujiandaa kwa mechi ya kwanza ya mchujo ya michuano
ya Afrika kwa vijana wenye umri chini ya miaka 17 dhidi ya Misri
itakayochezwa Oktoba 14 mwaka huu jijini Dar es Salaam.
KAMSHINA MMOJA AONDOLEWA KWENYE LIGI
Kamati ya Ligi ya Shirikisho la Mpira wa
Miguu Tanzania (TFF) ilikutana jana (Septemba 25 mwaka huu) kupitia
ripoti za mechi 21 za Ligi Kuu ya Vodacom ambazo zimeshachezwa mpaka
sasa, na kuzifanyia uamuzi wa kikanuni ikiwemo kumuondoa Kamishna mmoja.
George Komba aliyekuwa Kamishna kwenye
mechi namba 20 kati ya Simba na Ruvu Shooting ameondolewa kwenye orodha
ya makamishna wa ligi kutokana na upungufu uliojitokeza katika ripoti
yake.
Klabu ambazo zimeandikwa barua za onyo
ni African Lyon kwa kwenda uwanjani na jezi tofauti na zile ilizoonesha
kwenye mkutano wa maandalizi ya mechi (pre match meeting), Mtibwa Sugar
kwa kuchelewa kuwasilisha leseni za wachezaji wake wakati wa mechi na
Ruvu Shooting kwa ushangiliaji uliopita kiasi kwenye mechi yao dhidi ya
Simba.
Kamati pia imethibitisha kadi nyekundu
ya Emmanuel Okwi kwa kumpiga kiwiko Kessy Mapande wa JKT Ruvu, hivyo kwa
mujibu wa Kanuni ya 25(1)() anakosa mechi tatu na kulipa faini ya sh.
500,000. Mchezaji huyo atakosa mechi namba 20, 27 na 80.
Kwa upande wa waamuzi, Ronald Swai
ameandikiwa barua ya onyo kutokana na upungufu alioonesha kwenye mechi
kati ya Simba na Ruvu Shooting iliyochezwa Uwanja wa Taifa, Dar es
Salaam.
Wamiliki wa viwanja vya Mkwakwani, Tanga
na Kumbukumbu ya Sokoine, Mbeya wameandikiwa barua ya kuvifanyia
marekebisho viwanja vyao katika maeneo mbalimbali yenye upungufu ikiwemo
uzio wa kutenganisha wachezaji na washabiki.
Mchezaji Faustin Lukoo wa Polisi Moro
ambaye kwa mujibu wa ripoti ya mwamuzi aliyemtoa nje kwa kadi nyekundu
alimtukana mchezaji mwenzake kwenye mechi dhidi ya African Lyon na
Katibu wa Oljoro JKT aliyemwaga maji kwenye chumba cha timu ya Polisi
Moro, masuala yao ni ya kinidhamu, hivyo yamepelekwa Kamati ya Nidhamu
na Usuluhishi kwa ajili ya hatua zaidi.
Kwa klabu ambazo timu zao mpaka sasa
zinacheza mechi bila kuwa na logo ya mdhamini, suala hilo limepelekwa
kwa wadhamini Vodacom kwa vile wenyewe ndiyo wanaogawa vifaa hivyo.
TENGA KUKUTANA NA WAANDISHI KESHO SAA 6
Rais wa Shirikisho la Mpira wa Miguu
Tanzania (TFF), Leodegar Tenga atakutana na waandishi wa habari kesho
(Septemba 27 mwaka huu) saa 6 kamili mchana. Mkutano huo utafanyika
kwenye ukumbi wa mikutano wa TFF.
Boniface Wambura
Ofisa Habari
Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF)
No comments:
Post a Comment