Wednesday, 3 October 2012

MKUU WA MKOA WA MBEYA ABBASI KANDORO KANDORO KUWA MGENI RASMI SIKU YA MBEYA KWANZA SUPER BONANZA




 Mratibu wa Life Time Entertainment & Marketing Limited, Venance Matinya akitafakari jambo pamoja na baadhi ya wanahabari wa Mkoa wa Mbeya.
Na Emmanuel Madafa,Mbeya.
MKUU wa Mkoa wa Mbeya Abbasi Kandoro anatarajiwa kuwa Mgeni rasmi katika Bonanza lililoandaliwa na Kampuni ya Life Time Entertainment & Marketing Limited ya Mjini hapa, lenye lengo la kuwakusanya watu wengi kwa ajili ya kuhamasisha maendeleo ya Mkoa wa Mbeya.
Akitoa taarifa kwa vyombo vya Habari katika Mkutano uliofanyika jana kwenye ukumbi wa Hoteli ya Mount Living Stone ya Mjini hapa, Mratibu wa kampuni hiyo, Venance Matinya alisema   Bonanza hilo litahusisha Taasisi za Umma, Mashirika Binafsi, Wanahabari wa Mkoa wa Mbeya na Wadau mbali mbali wapenda maendeleo ya Mkoa wetu.
Amesema Bonanza hilo  litaitwa “Mbeya Kwanza Super  Bonanza” ambalo litakuwa na lengo la  kuwakutanisha waandishi wa habari na wadau mbali mbali ili kuhamasisha uwekezaji wa ndani na vivutio vya mkoa wa Mbeya na kukemea dhana potofu juu ya vitendo vya upigaji nondo na ushirikina vinavyosababisha kukwamisha maendeleo ya Mbeya.
“ Bonanza letu litakuwa na Ujumbe unaosema “ pinga vitendo vya ukatili, migogoro ndani ya jamii, epuka uvunjifu wa amani hamasisha amani na uzalendo katika mkoa wa Mbeya na Tanzania”hivyo ndugu zangu tusaidiane kuhamasisha uzalendo wetu” alisema.
Ameongeza kuwa  kutokana na umuhimu wa Bonanza hilo Mkuu wa Mkoa wa Mbeya Abbasi Kandoro amekubali kushiriki na kuwa mgeni rasmi katika bonanza litakalofanyika siku  ya  Jumamosi Oktoba 20, mwaka huu katika viwanja vya shule ya msingi Ruanda Nzovwe.
Mratibu huyo amesema katika bonanza hilo litakaloanza mapema asubuhi litakuwa na michezo mbali mbali kama vile Mpira wa miguu(wanaume),netboli(wanawake),kuvuta kamba na riadha kukimbiza kuku na kuvuta kamba.
“Pia katika ratiba yetu tutakuwa na hotuba mbali mbali ambazo zitatolewa siku hiyo ambazo zikuwa na ujumbe wa kuhamasisha uwekezaji wa ndani itakayotolewa na uongozi wa kituo cha uwekezaji kanda ya Nyanda za juu kusini.
Na kuongeza kuwa, hotuba nyingine itatolewa na Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mbeya ambaye atakemea uhalifu na kuhamasisha amani na utulivu, Mwenyekiti wa Mjata ambaye atakemea vitendo vya ushirikina na kujipatia mali kwa njia za udanganyifu vitendo vinavyosababisha kukosekana kwa maendeleo katika mkoa wetu” alisema Matinya.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Kampuni hiyo, Humphrey Masassi ametumia nafasi hiyo kutoa  wito kwa makampuni mbali mbali kujitokeza kutoa udhamini kwenye matukio yanayo hamasisha maendeleo ya eneo husika na siyo kusubiri watu wan je kuja kufanya biashara ndani ya mkoa wa Mbeya.
Masassi amesema Mkuu wa Mkoa pia atatoa hotuba pamoja na kutoa zawadi kwa washiriki wa bonanza hilo wakiwemo wanahabari ambapo pia muda huo utatumika kwa ajili ya Benki ya damu salama kutoa elimu kwa washiriki ili waweze kuchangia damu kwa ajili ya wenzetu walionauhitaji kutokana na ajali nyingi zinazoendelea kutokea maeneo mbali mbali.
Ameongeza kuwa Mbali na Bonanza hilo pia Kampuni yake  Kwa kushirikiana na SAM ENTERTAINMENT imeandaa uzinduzi wa Filamu inayoitwa KIJAKAZI ambayo itazinduliwa Oktoba 5 Mwaka huu siku ya Ijumaa katika ukumbi wa Mkapa ulioko Sokomatola Jijini Hapa ambapo uzinduzi huo utasindikizwa na wasanii kutoka Dar kama vile Senga na Pembe.

No comments: