Wednesday, 3 October 2012

Polisi Moshi Yatangaza Kiama Cha Makahaba



Na: Daniel Mjema, Moshi, Mwananchi. 

POLISI imeanzisha operesheni kaMambe ya kupambana na biashara ya ukahaba Mji wa Moshi na tayari wanawake zaidi ya 150 wanaouza miili yao wametiwa mbaroni. Hata hivyo, wanawake hao wengi wao wakitokea kata za Njoro, Pasua, Majengo, Kaloleni, Korongoni na Kwamtei wamekuwa wakirejea katika mawindo yao baada ya kuachiwa kwa dhamana na mahakama. Vifungu 145,146 na 147 vya kanuni ya adhabu cape 16 kama vilivyofanyiwa marejeo mwaka 2002, vinaharamisha biashara ya ukahaba siyo kwa mwanamke tu, hata mwanamme anayefanya nao mapenzi.

 Ingawa vifungu hivyo havijaweka adhabu, lakini vikisomwa pamoja na kifungu namba 35 cha sheria hiyo, inatamka bayana kuwa mtuhumiwa anaweza kufungwa miaka miwili jela, faini au vyote viwili. Pia, chini ya sheria hiyo anayegeuza nyumba yake au chumba chake au eneo lake kwa njia yoyote ile ili litumike kwa shughuli za ukahaba, anatenda kosa na anaweza kufungwa hadi miaka miwili jela. 

 Hata hivyo, baadhi ya wanawake hao wamekuwa wakifikishwa mahakama ya mwanzo na kushtakiwa kwa kosa la uzururaji, kutokana na kukosekana kwa ushahidi wa moja kwa moja wa kosa la ukahaba. Wanawake waliolengwa katika operesheni hiyo kali kuwahi kufanywa na polisi, ni wale wanaojipanga hadharani karibu na klabu mashuhuri za usiku kusubiria wateja hadi usiku wa manane.

 Uchunguzi zaidi umebaini kuwa kutokana na kashkashi hiyo, wanawake hao sasa wamebuni mbinu mpya ambapo huingia ndani ya klabu hizo na kukaa kama wateja wakiwa na chupa za bia zenye maji. 

 Baadhi ya wateja wakiwamo wanaume walioko kwenye ndoa, nao wamebuni mbinu mpya ambapo ‘humalizana’ na wanawake hao kwenye magari wanayoegesha kwenye giza nje ya klabu hizo. 

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kilimanjaro, Robert Boaz alithibitisha kuendelea kwa operesheni hiyo akisema ilianza wiki nne zilizopita na itakuwa endelevu hadi vitendo hivyo vitakapokoma.

No comments: