TAASISI ya kuzuia na kupambana
na Rushwa (TAKUKURU) Mkoa wa Mbeya, imemfikisha mahakamani Mhasibu wa
Halmashauri ya Wilaya ya Mbeya kwa kosa la kuhujumu uchumi na Rushwa.
Mtumishi huyo alifikishwa jana
mbele ya Hakimu Mkazi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Mbeya, James Mhanusi chini ya
Mwendesha mashtaka wa Takukuru, Nimrod Mafwele.
Mwendesha mashtaka wa Serikali
Nimrod Mafwele alimtaja mshtakiwa kuwa ni Geshon Bwile ambaye ni mhasibu wa
Halmashauri hiyo akituhumiwa kwa makosa matatu aliyoyatenda Mei 2, 2013.
Aliyataja makosa hayo kuwa ni
pamoja na kutumia Nyaraka za Serikali kujipatia fedha kinyume cha kifungu cha
22 cha Sheria ya Takukuru namba 11 ya mwaka 2007.
Alisema katika kosa hilo
Mtuhumiwa akiwa ni mhasibu wa Halmashauri ya Wilaya ya Mbeya alitumia risiti
yenye namba 0009 kumwandikia Rich & Mr&Mrs Mufat Decoration kwa malipo
ya mapambo yenye thamani ya shilingi Milioni 1,350,000 wakati sio kweli.
Mwendesha mashtaka huyo alilitaja kosa lingine
kuwa ni Ubadhilifu kinyume cha kifungu
cha 28(1) namba 11 cha mwaka 2007 ambapo alijipatia kiasi cha shilingi Milion
1,350,000 alichokabidhiwa na Halmashauri ya Wilaya ya Mbeya.
Alilitaka kosa la tatu kuwa ni
kuisababishia hasara mamlaka kinyume cha
Sheria kifungu cha 10(1),(i),57(1) na 60(2) ya uhujumu uchumi namba 200
iliyofanyiwa marejeo mwaka 2002, ambapo Halmashauri ilipata hasara ya shilingi
Milion 1,350,000 mali ya Jamhuri ya muungano wa Tanzania.
Baada ya kusomewa mashtaka yote
hayo Mtuhumiwa alikataa yote ambapo upande wa mashtaka ulisema upelelezi
umekamilika na kuomba tarehe nyingine kwa ajili ya kusikiliza maelezo ya awali.
Aidha mshtakiwa aliachiwa kwa
dhamana baada ya kukamilisha masharti ambayo ni kuwa na wadhamini wawili ambao
ni watumishi wa Serikali wakiwa na barua kutoka kwa mwajiri,mali kauli ya Shilingi
Milioni Moja kila mmoja.
Hakimu Mhanusi alisema
mashariti mengine ni kutokana na kifungu cha 148 (6) ambapo mtuhumiwa harusiwi
kutoka nje ya Mkoa wa Mbeya bila ruhusa ya mahakama pamoja na kuwasilisha hati
ya kusafiria kwenye kituo cha polisi jambo ambalo aliyatimiza papo hapo.
Hata hivyo kesi hiyo
iliahirishwa hadi Julai 25 mwaka huu ambapo mtuhumiwa ataanza kusomewa maelezo
ya awali na kuendelea kusikiliza upande wa mashahidi.
Kesi hiyo ni ya pili kwa TAKUKURU
Mkoa wa Mbeya kuwafikisha Mahakamani watumishi wa Halmashauri ya Mbeya baada ya
hivi karibuni kumfikisha Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Mbeya, Upendo
Sanga, na Watumishi wengine kwa kosa la kuhujumu uchumi.
No comments:
Post a Comment