Friday, 4 July 2014

UJENZI WA NJIA ZA KUPITISHIA WAGONJWA HOSPITALI YA MKOA WA MBEYA WAENDELEA KWA KASI.


Mwenyekiti wa Kamati ya Marafiki wa Hospitali ya Mkoa wa Mbeya, Oleais Senga,akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake kuhusu maendeleo ya ujenzi huo.



Mganga Mfawidhi wa Hosipitali ya Mkoa wa Mbeya, Dk. Grolia Mbwile, akielezea jinsi ujenzi huo unavyoendelea kwa kasi






UJENZI wa njia za kupitishia wagonjwa katika Hospitali ya Mkoa wa Mbeya unaendelea kwa kasi inayotokana na  mkandarasi aliyejitolea kujenga bure kuonesha uwezo wake.
Kutokana na kasi hiyo uongozi wa Hospitali, umetoa pongezi na kuishukuru kamati ya  marafiki wa Hospitali hiyo kwa kufanikisha upatikanaji wa fedha za kuanzia.
Pongezi  hizo zimetolewa na Mganga Mfawidhi wa Hosipitali ya Mkoa wa Mbeya, Dk. Grolia Mbwile, wakati akizungumza na mtandao wa Mbeya yetu uliotembelea Hospitalini hapo kwa lengo la kujua kama ujenzi huo umeaanza na  maendeleo yake.
Dk. Mbwile amesema ujenzi unaendelea kwa kasi kubwa hivyo wanaopaswa kupewa shukrani ni kamati ya marafiki wa Hospitali waliotoa wazo na kuanza kuchangishana fedha na hatimaye zoezi la ujenzi kufanyika.
Amesema bila marafiki hao bado wagonjwa wangeendelea kuteseka kwa kushindwa kuvuka Wodi moja hadi lingine kutokana na kukosekana kwa miundombinu mizuri ya kuwapitishia wagonjwa.
Amesema hufikia wakati mgonjwa anapaswa kusukumwa kwa toroli maalumu kutoka chumba cha daktari hadi Wodini lakini hushindikana kutokana na kutokuwepo kwa njia maalumu za kupitia.
 Dk Mbwile ametoa wito kwa wananchi mbali mbali wenye uwezo wa kuchanga chochote akafanya hivyo ili kufanikisha ujenzi huo kukamilika kwa wakati unaotakiwa.
Amesema sio lazima mtu akatoa fedha bali anaweza kujitolea Mchanga, Kokoto, Sementi, Misumari,Mbao, Vyuma na mabati ambavyo kwa namna moja ama nyingine vitarahisisha matumizi ya fedha kupungua.
Naye Mkandarasi atakayesimamia Ujenzi huo, Mhandisi Wilson Mwangonela amesema endapo fedha zote zinazohitajika ambazo ni Shilingi 240,877,575 zitakuwepo zote ujenzi huo unaweza kukamilika ndani ya Wiki tatu hadi nne.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Kamati ya Marafiki wa Hospitali ya Mkoa wa Mbeya, Oleais Senga, amesema hadi sasa wameshakusanya zaidi ya Shilingi Milion 40.
Ameongeza kuwa wakati fedha zingine zikisubiriwa kukamilishwa kwa walioahidi ni vema wadau wengine wakajitokeza kuchangia fedha zilizosalia ili kufanikisha ujenzi wa miundombinu ya kupitishia wagonjwa kwa njia ya vitanda vyenye magurudumu.
Amesema ujenzi huo utafanywa na Mkandarasi wa kampuni ya Inter Frempa Co.Ltd yenye makao makuu jijini Mbeya pamoja na Chuo kikuu cha Sayansi na Teknolojia(MUST) waliojitolea kuchora ramani ya ujenzi huo bure bila malipo yoyote.
Amesema kujitolea kwa watu hao kumepunguza baadhi ya gharama na kurahisisha ujenzi na kutoa wito kwa wadau kujitoa kwa hali na mali ili ujenzi huo ukamilike kwa wakati kupitia Mpesa 0762 321829 yenye jina la Marafiki Mkoa au akaunti namba 0150067027600 CRDB jina Marafiki wa Hospitali ya Mkoa wa Mbeya.

No comments: