Tuesday, 5 May 2015

Mateso...!......Mateso...! Mgomo wa Madereva Wakwamisha Maelfu ya Abiria



MGOMO wa mabasi ulioibuka jana, umeitikisa nchi kiasi cha kusimamisha shughuli nyingi na kusababisha adha kwa wadau katika sekta nzima ya usafirishaji.
 
Mbali ya abiria waliokuwa wasafiri ndani na nje ya nchi kutoka Kituo Kikuu cha Mabasi Ubungo na kwingineko nchini, wanafunzi wa Kidato cha Sita walioanza mitihani yao jana, baadhi yao waliathirika kwa kushindwa kufika kwa wakati katika vituo vyao vya mitihani.
 
Aidha, abiria katika Kituo cha Ubungo, wakionekana kukata tamaa huku muda mwingi wakinyeshewa na mvua kituoni hapo ambako hakuna sehemu za kutosha za kupumzikia abiria, walijikuta wakivamia Kituo Kidogo cha Polisi na kuanza kufanya fujo, wakitaka waonyeshwe mahali pa kula na kulala.
 
Abiria wengine walitoka nje ya kituo na kwenda kufunga barabara ya Morogoro, hali iliyowalazimu askari wa Jeshi la Polisi kutumia nguvu kiasi, ikiwa ni pamoja na kufyatua mabomu ya machozi kwa lengo la kuwatawanya.
 
Hali ilivyokuwa Ubungo
Katika Kituo Kikuu cha Ubungo, licha ya abiria kumiminika tangu alfajiri, wengine wakiwa na tiketi mikononi mwao, hawakuweza kusafiri kwani madereva na wasaidizi wao hawakuonekana, huku mabasi yakiwa yameegeshwa kituoni hapo.
 
Kituo cha mabasi Ubungo kinatumiwa na zaidi ya mabasi 600 kwa siku. Abiria walijikuta katika wakati mgumu huku mvua ikinyesha bila ya kujua hatma ya safari zao huku wengi wao wakiwa na tiketi wakiwa wamekaa ndani ya mabasi wakionekana kukata tamaa ya kusafiri.
 
Wakati abiria wakitafakari juu ya hatima ya safari zao, madereva wa mabasi, daladala na malori walikusanyika Ubungo kupanga mambo yao na pia kuchangishana fedha ambazo hazikuelewa zilikuwa za nini.
 
Miongoni mwao, huku wakiwakacha wanahabari na kuwataka waondoke eneo hilo, walibeba mabango yaliyokuwa yameandikwa, “Tanzania Bila Mgomo wa Madereva Inawezekana, Tunahitaji Mikataba Bora ya Kazi.”
 
Hata hivyo, baadhi ya wafanyakazi katika ofisi za kukatia tiketi kituoni hapo waliendelea kuwahamasisha abiria kuendelea kukata tiketi wakiamini suala hilo litafikia tamati, hasa baada ya kuelezwa mambo yatakwisha baada ya mkutano wa viongozi wa madereva na Waziri Mkuu, Mizengo Pinda ofisini kwake.
 

Askari wa Kikosi cha Usalama barabarani, Solomon Mwangamilo, akijaribu kutoa moja ya mabasi yaliyokuwa kwenye mgomo  katika Kituo cha Mabasi Ubungo jijini Dar es Salaam.
Lakini tofauti na matarajio ya wengi, mtandao huu ulidokezwa kuwa, mkutano huo haukufanyika kwa kile kinachoelezwa baadhi ya madereva waliwadhibiti viongozi wao wasionane na Waziri Mkuu, wakishinikiza aende kuzungumza na madereva wote Ubungo.
 
Awali, katika eneo la kituo cha mabasi ya mikoani Ubungo, Katibu Mkuu wa Umoja wa Madereva Tanzania, Rashid Saleh alisema ni kweli kuwa wamepokea taarifa ya viongozi wa madereva kwenda kuonana na Waziri Mkuu na kwa muda huo (saa 6:30 mchana) walikuwa wakijipanga.
 
Alisema taarifa hiyo waliipokea kutoka kwa Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Said Meck Sadiki na kwamba watakwenda ili kupeleka madai yao na kama hayatofanyiwa kazi kama wanavyotaka watazidi kupumzika.
 
“Kwa leo hadi muda huu saa sita tumewaambia madereva waende wakapumzike kwa kuwa tutawapa majibu jioni baada ya kuonana na Waziri Mkuu,” alisema Rashid.
 
Kutokana na mgomo huo hakuna basi hata moja lililoondoka wala kuingia kituoni hapo. Aliongeza kuwa wana matatizo makubwa na waajiri wao kuhusu suala la mikataba na kuitaka serikali kuwabana waajiri ili waweze kupata mikataba iliyo bora.
 
Awali, Kamanda wa Kikosi cha Usalama Barabarani nchini, Mohammed Mpinga, alifika kituoni hapo saa 3 asubuhi na kuingia ndani ya kituo kidogo cha Polisi akionekana kujadiliana na askari Polisi waliokuwa kituoni hapo kisha kuondoka na kudai kuwa hawezi kuzungumza jambo lolote kwa kuwa mambo bado magumu na kwamba Waziri Mkuu atafika kituoni hapo majira ya saa sita mchana.
 
Askari  wakiwa wamemkamata mmoja wa vijana waliokuwa wakizuia magari kupakia abiria katika eneo la Ubungo, baada ya madereva wa mabasi kugoma jijini Dar es Salaam jana
Muda mfupi kabla ya kuwasili kwa Mpinga, mmoja wa askari aliyefahamika kwa jina la Solomon Mwangamilo aliingia ndani ya basi la Master City, huku likiwa na abiria aliliendesha hadi nje ya kituo cha mabasi, karibu na mataa ya Ubungo kwa lengo la kumshinikiza dereva aendelee na safari yake.
 
Hata hivyo, inaelezwa kuwa dereva wa basi hilo alitokomea kusikojulikana akiogopa kuonekana msaliti kwa wenzake, jambo lililomlazimu Solomon kurejesha basi hilo ndani ya kituo.
 
Adha kama hizo hazikuwakuta abiria wa mabasi ya mikoani tu, bali hata watumiaji wa daladala waliojikuta wakitembea kwa miguu kwa umbali mrefu, kwani hakukuwa na usafiri, na wachache waliobahatika kupata bodaboda au magari ya mizigo aina ya Suzuki Carry maarufu kama `Kirikuu’, walitozwa nauli za juu.
 
Kwa ujumla, katika siku ya jana magari ya Kirikuu ndiyo yaliyotamba kwa kusafirisha abiria, sawa na bodaboda. Inaelezwa kwa magari binafsi, nauli ya chini ilikuwa Sh 2,000 ilhali kwa usafiri wa daladala, nauli ni kati ya Sh 400 na 500, ikitegemea umbali.
 
Kwa wanafunzi, hutozwa Sh 200, lakini jana wote walilipishwa sawa na watu wazima. Hali hiyo imeelezwa kuathiri baadhi ya wanafunzi wa Kidato cha Sita walioanza mitihani yao jana.Takribani watahiniwa 40,758 walianza mtihani yao ya mwisho ya kuhitimu Kidato cha Sita.
 
Serikali kusaidia Kidato 6
Kutokana na adha hiyo, Serikali imesema itaweka utaratibu maalumu wa kufanya mitihani kwa watahiniwa watakaokuwa wamechelewa mitihani ya asubuhi kutokana na mgomo wa mabasi ya abiria.
 
Hayo yamesemwa na Waziri mwenye dhamana ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Dk Shukuru Kawambwa.
 
Akizungumza wakati wa mahojiano kupitia kipindi cha Asubuhi Hii kinachorushwa na kituo cha Redio ya Taifa cha TBC Taifa, Dk Kawambwa alisema kama kutakuwepo na taarifa ya wanafunzi kushindwa kufanya mitihani yao kutokana na mgomo wa usafiri, wataweka utaratibu wa wanafunzi hao kufanya mitihani hiyo waliyoikosa.
 
Tunajua kuwa kuna baadhi ya wanafunzi wako bweni wengine wa kutwa, na tukipokea taarifa kutoka kwa wasimamizi wa vituo kuwa wanafunzi wamechelewa kufanya mitihani na tutaangalia sababu na kama imetokana na mgomo wa usafiri basi tutawawekea utaratibu wa kuifanya hiyo waliyoikosa,” alisema.
 
Jana asubuhi, watahiniwa hao walitakiwa kufanya mtihani ya Hisabati na Kiswahili na mchana walitakiwa kufanya Mtihani wa Maarifa.
 
Chanzo cha mgomo
Madereva hao wamegoma wakidai haki zao za msingi ikiwa ni pamoja na kufutwa kwa hatua ya kusoma kila baada ya leseni kuisha, mikataba bora, posho za safari na mishara inayokidhi malipo na bima kwa dereva.
 
Hii ni mara ya pili kwa madereva hao kufanya mgomo, kwani Aprili 10, mwaka huu, waligoma na kusababisha adha kubwa ikiwa ni pamoja na kuyumbisha shughuli za kiuchumi na kijamii karibu nchi nzima.

No comments: