Sunday, 3 May 2015

MBOWE: JUHUDI IFANYIKE KUNUSURU SHILINGI


Mwenyekiti wa Taifa wa Chadema, Freeman Mbowe
Mwenyekiti wa Chama cha Maendeleo (Chadema), Freeman Mbowe
MWENYEKITI wa Chama cha Maendeleo (Chadema), Freeman Mbowe ameomba serikali kufanya juhudi za kunusuru Shilingi isiendelee kushuka.
Pia ametoa mwito kwa Kamati Kuu ya Chadema iliyo kwenye kikao chake, kujadili na kutoa maoni yao juu ya nini kifanyike ili kunusuru Shilingi na uchumi wa nchi.
Mbowe alisema hayo jana jijini Dar es Salaam wakati wa ufunguzi wa kikao cha Kamati Kuu, inayokutana kwa siku mbili. Hata hivyo, kwa upande wake, Benki Kuu ya Tanzania (BoT) imesema tayari imeshaanza kuchukua hatua za kudhibiti kuporomoka kwa kasi kwa Shilingi.

Akizungumza na gazeti hili mwishoni mwa wiki, Mkurugenzi wa Fedha na Masoko wa BoT, Alexander Ng'winamila, alisema kamwe Serikali haiwezi kukalia kimya suala hilo.
"Tumeshaanza kuchukua hatua ya kudhibiti hali hii, na tumeanza na hatua ya kuuza dola kwenye soko, hii itatusaidia kuipandisha Shilingi," alisema.
Mbowe alifafanua kuwa ni lazima itafutwe suluhu ya kuhakikisha thamani ya Shilingi inaimarika, kwani kuendelea kushuka kwake kunahatarisha hata masuala ya uwekezaji.
"Ni lazima hatua zichukuliwe kunusuru, kuporomoka kwa thamani ya Shilingi, kwani hali hii inadhoofisha ukuaji wa uchumi wetu, na kamati kuu niwaombe nanyi tafakarini mtoe maoni yenu ya nini cha kufanya kunusuru uchumi wa nchi yetu", alisema Mbowe.
Alisema thamani ya Shilingi nchini imeshuka thamani kwa shilingi zaidi ya nne ndani ya miezi michache, na hali hiyo sio njema kwa ukuaji wa uchumi, kwa kuwa inachangia pia miradi mikubwa kusimama kwa sababu ya hofu ya sarafu kushuka thamani.
Aliishauri serikali kuangalia mbinu za kukabiliana na kushuka kwa thamani ya Shilingi nchini, ili kusije kuharibu uchumi na kuongeza hali ngumu kwa wananchi wa kipato cha kawaida.
Mbowe pia aliishauri kamati kuu hiyo, kujadili kwa kina hali ya kisiasa nchini wakati wa harakati za uchaguzi mkuu, pamoja na kujadili na kuja na maoni yao jinsi ya kuendelea kukiongoza chama.CHANZO: HABARI LEO 

No comments: