Wednesday 6 May 2015

MGHANA MPYA SIMBA NOMA SANA

Mshambuliaji wa Simba raia wa Ghana, Aboagye Gerson.
Wilbert Molandi na Sweetbert Lukonge

WAKATI mchakato wa usajili wa kimyakimya ukiendelea kwa ajili ya msimu ujao wa Ligi Kuu Bara, Simba jana ilimshusha mshambuliaji raia wa Ghana, Aboagye Gerson aliyekuwa anakipiga Klabu ya Zhako ya Iraq.
Ujio wa Mghana huyo ni mipango ya kukiboresha kikosi hicho katika kuelekea msimu ujao baada ya Kocha Mkuu wa Simba, Goran Kopunovic kutoa mapendekezo ya usajili wa mshambuliaji mmoja anayejua kazi yake inavyotakiwa.(P.T)
Simba imekuwa ikikosa mshambuliaji mwenye makali tangu alipoondoka Amissi Tambwe mwanzoni mwa msimu huu huku Dan Sserunkuma aliyeziba pengo akishindwa kuwa hatari katika ufungaji.
Mghana huyo, anayecheza nafasi ya ushambuliaji namba tisa, alikuwa mmoja wa walioshiriki katika mazoezi ya timu hiyo yaliyofanyika kwenye Uwanja wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam kwa ajili ya majaribio kabla ya kupewa mkataba.
Straika huyo alionyesha uwezo mkubwa katika kumiliki na kupiga pasi katika muda wa saa moja na nusu alizopewa mazoezini hapo.
Alipiga mashuti makali kiasi cha kusababisha mashabiki waliojitokezauwanjanihapo kujiuliza mchezaji huyo ametokea wapi.Aidha, alionyesha uwezo mkubwa wa kumiliki mpira na kumpa tabu beki Mganda, Juko Murshid aliyekuwa akimkaba.
Alipoulizwa Kopunovic juu ya mchezaji huyo alisema: “Nimemuona kwa muda mfupi, ni ngumu kuzungumzia uwezo wake, lakini kwa kifupi tu bado ninahitaji muda wa kumuangalia.
“Siku mbili au tatu kwangu hazinitoshi kujua uwezo wake na kushawishi kutoa mapendekezo ya kumsajili, ninaomba muda zaidi, isitoshe kipindi hiki siyo kizuri kwangu kwa ajili ya kuangalia wachezaji wakati tukiwa tupo kwenye ligi,” alisema Kopunovic.Mshambuliaji huyo naye alisema: “Hiki siyo kipindi changu cha kuzungumza, kwa kifupi nimekuja kwa ajili ya majaribio.”

No comments: