Monday, 4 May 2015

Ruto: Mashoga na wasagaji hawana nafasi Kenya

Ruto: Wasenge na wasagaji hawana nafasi Kenya


Makamu wa Rais wa Kenya, William Ruto amesema kuwa, wasenge na wasagaji hawana nafasi katika nchi hiyo ya Afrika Mashariki.

 Ruto ameyasema hayo  jijini Nairobi ambapo ameonyesha kusikitishwa kwake na ongezeko la idadi ya wasenge na wasagaji katika nchi kadhaa za Kiafrika katika siku za hivi karibuni. Makamu wa Rais wa Kenya amesema kuwa, serikali ya Nairobi, haitaruhusu vitendo hivyo katika jamii ya nchi hiyo na kwamba vinakinzana na utamaduni wa Wakenya na Waafrika.

 Aidha amesisitiza kuwa, msimamo wa serikali katika kupiga vita usenge na usagaji nchini Kenya sio suala la kisiasa wala si kwa ajili ya kuvutia kura za wananchi katika uchaguzi, bali ni wadhifa wa kisheria na kikatiba. Kauli hiyo ya Makamu wa Rais wa Kenya, William Ruto ya kulaani vitendo hivyo, imetolewa siku chache tu baada ya Mahakama Kuu nchini humo kusalimu amri mbele ya mashinikizo ya watetezi wa vitendo hivyo vichafu vya ulawiti na usagaji na kusema kuwa sasa watu wanaojihusisha na vitendo hivyo wanaweza kusajili chama chao serikalini kwa kile kinachodaiwa ni kutetea haki zao za kibinadamu. 

Uamzi huo ulichukuliwa ikiwa kumesalia mwezi mmoja kabla ya safari ya Rais Barack Obama wa Marekani nchini Kenya ambaye ni mtetezi mkuu wa vitendo hivyo vichafu.

No comments: