WAJUMBE wa Baraza la Mji Mdogo wa Tunduma wilayani Momba, Mkoa wa Mbeya, juzi nusura wachapane makonde baada ya kushindwa kuelewana walipokuwa kwenye kikao chao.
Tukio hilo lilidumu kwa dakika zipatazo kumi likiwahusisha wanachama wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) na wanachama wa Chama Cha Mapinduzi (CCM).
Kabla ya tukio hilo, awali Ofisa Mipango wa Mji huo, Mutta Bahenobi, alitaka ufafanuzi wa matumizi ya eneo la Sogea lililotengwa kwa ajili ya ujenzi wa majengo ya umma.
Katika mazungumzo yake, Bahenobi alionyesha kupingana na wajumbe wa baraza hilo wanaotoka CCM ambao wamekuwa wakisema eneo hilo ni mali ya chama chao.
“Kumbukumbu zinaonesha kuwa eneo la Sogea limetengwa kwa ajili ya matumizi ya umma na siyo mali ya chama fulani kama baadhi ya watu wanavyosema,” alisema Bahenobi.
Baada ya maelezo hayo, baadhi ya wajumbe kutoka CCM walimpinga Ofisa Mipango huyo hali iliyosababisha wajumbe wenzao kutoka Chadema waingilie kati wakionyesha kuungana na Bahenobi.
Wakati wa mabishano hayo, Mwenyekiti wa Baraza hilo, Salvatory Ngole (Chadema), aliungana na kauli ya Bahenobi akisema ramani iliyopo inaonyesha eneo hilo limetengwa kwa ajili ya ujenzi wa majengo ya umma na siyo mali ya chama chochote cha siasa.
Awali, akizungumza kwa niaba ya Mkuu wa Wilaya ya Momba, Richard Mbeho, Ofisa Utumishi wa Wilaya hiyo, Mathias Mizengo, aliwataka wajumbe wa baraza hilo kusimamia maendeleo katika maeneo yao ili wananchi waweze kuwaamini.
No comments:
Post a Comment