Waziri wa nishati na madini Mh.George Simbachawene ameagiza kusimamishwa kazi mara moja kwa wahandisi watatu wa shirika la umeme nchini TANESCO kutoka maeneo matatu jijini Dar es salaam baada ya wahandisi hao kushindwa kuwajibika ipasavyo ikiwa ni pamoja na kutochukua hatua wanapopewa taarifa za kero za wananchi kwenye maeneo wanayosimamia
Wahandisi hao ni wa Temeke, Tazara na Tabata Magengeni, jijini Dar es Salaam, wanaodaiwa kusababishia Shirika hilo malalamiko kutoka kwa wananchi kila wakati.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana, Simbachewene alisema baadhi ya malalamiko yanayotolewa na wateja ni taarifa wanazotoa kuhusu nyaya za umeme na nguzo kuanguka bila kuchukuliwa hatua zozote.
Simbachewene alisema wajibu wa watendaji hao ni kushughulikia kero kama hizo sio wananchi waende kulalamika.
"Kila kukicha wanalalamikiwa Tanesco jana nilipiga simu Tazara na Tabata kuwajulisha kuna tatizo lakini hawajaenda, unakuta nyaya ya umeme imeanguka ina maana inasubiria fedha ya kigeni ndio itolewe hivi kazi yenu nini? Nguzo imeanguka mnajulishwa mwezi unapita hilo gari la emergency linafanya kazi gani," alihoji.
"Huyo mhandisi wa Tabata inawezekana hata hajui kitu, matatizo ni mengi na sidhani kama anafika na kuyafuatilia, hivyo naagiza chukueni hatua za kinidhamu ili iwe fundisho na kwa wengine," alisema.
Akizungumzia kero za kukatika umeme mara kwa mara alisema, umeme unakatika pasipo na sababu maalum. Waya umeanguka Temeke hadi watu wanakufa hakuna hatua zilizochukuliwa.
“Wananchi wamepiga simu hakuna hatua zilizochukuliwa mpaka watu wanakufa hatuwezi kuyanyamazia haya," alisema na kuongeza:
“Sisi ni watumishi wa watanzania kwa leo naaza na hawa watatu wanatosha, wengine nitaendelea nao.”
“Sisi ni watumishi wa watanzania kwa leo naaza na hawa watatu wanatosha, wengine nitaendelea nao.”
Aidha, amepiga marufuku uegeshwaji wa magari ya Tanesco katika maeneo ya starehe kama baa, jambo ambalo alisema linalalamikiwa na wananchi.
Aliagiza vibarua wote walikokuwa wakitumiwa kwenye gari la dharura la Tanesco, kuajiriwa ili wasiwe wanachukua rushwa kwa wateja.
Alisema vibarua hao wamefanyakazi kwa muda mrefu bila kupewaajira na kila wakati ajira za Tanesco zinatangazwa.
Kuhusu tatizo la Luku, alisema hali imerudi kama kawaida na kuwataka kuendelea kununua huduma hiyo kupitia mitandao yote ya simu nchini.
Alisema chazo cha tatizo ni moja ya kampuni ya uwakala wa kuuza Luku kusimamishwa kutokana na kutokidhi viwango matakwa na taratibu za Mamlaka za Mapato (TRA),
Alifafanua kuwa kusimamishwa kwa kampuni hiyo kulilazimu mauzo yote yaliyokuwa yanapitia kampuni hiyo yapitie kwenye kampuni nyingine.
Alisema ili kukabiliana na hali hiyo, kampuni za simu zinazotoa huduma hiyo zililazimika kujiunga na mitandao mingine inayotoa huduma hiyo.
Alisema kwa sasa tatizo hilo limeshughulikiwa na huduma hiyo imeanza kutolewa kama kawaida.
Aidha, alisema mpango wa kujiunga na kampuni nyingi zaidi zinazotoa huduma hiyo unafanyika ili kuondoa ukiritimba.
Akizungumzia azma ya kampuni ya Selcom ya kuishitaki Tanesco kwa kuvunja mkataba, alisema suala hilo haliwahusu kwani lipo upande wa TRA pamoja na Selcom.
No comments:
Post a Comment