Zanzibar.
Mawaziri wa Serikali ya Umoja wa Kitaifa (SUK) na Wawakilishi kutoka
CUF jana walitoka kwenye kikao cha bajeti cha Baraza la Wawakilishi,
wakipinga urasimu katika utoaji vitambulisho vya ukazi wa Zanzibar na
uandikishaji wapigakura.
Muda
mfupi baada ya tukio hilo, Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ)
ilitoa taarifa yake ikisema kitendo cha mawaziri wa CUF kutoka kwenye
kikao cha bajeti ni kuvunja katiba, kwa kuwa wameshindwa kuheshimu kiapo
cha utii katika utekelezaji wa majukumu yao, kwa mujibu wa Katiba ya
Zanzibar ya Mwaka 1964.
Mawaziri
hao walitoka nje ya kikao hicho muda mfupi baada ya Waziri wa
Miundombinu na Mawasiliano, Juma Duni Haji kusimama na kutoa malalamiko
ya kutoridhishwa na utendaji wa SUK katika kusajili na kutoa
vitambulisho hivyo vinavyotumika katika kuandikisha wananchi kwenye
Daftari la Wapigakura.
Wakati
wawakilishi hao wanaondoka ndani ya ukumbi, wenzao wa CCM walikuwa
wakipiga makofi huku wakiimba “CCM, CCM, CCM”, na baadaye baraza
kuendelea na muswada wa kupitisha mapato na matumizi ya bajeti ya mwaka
2015/2016.
Mawaziri
waliohudhuria mkutano huo ni Abubakar Khamis Bakar ambaye ni Waziri wa
Sheria na Katiba, Fatma Abdulhabib (Nchi, Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa
Rais), Abdilahi Jihadi Hassan (Mifugo na Uvuvi) na Haji Mwadini Makame
(Ardhi, Makazi, Maji na Nishati).
“Tumeamua
kutoka ndani baada ya kuona wenzetu tuliowaamini, wametubadilikia.
Hawana nia njema ya kuendesha serikali ya pamoja,” alisema makamu
mwenyekiti wa CUF, Juma Duni Haji alipoongea na waandishi baada ya
kutoka kwenye ukumbi huo.
“Wameanzisha Serikali ndani ya Serikali na sasa wanawanyima haki wananchi kinyume na katiba.”
Duni
alisema kwa miaka mingi wananchi wamekuwa wakizungushwa kusajiliwa na
kupewa vitambulisho vya ukazi, hali inayowaweka katika hatari ya
kupoteza haki zao za kijamii, ikiwa ni pamoja na fursa ya kushiriki
Uchaguzi Mkuu.
Hata hivyo, alisema uamuzi wao haujavunja katiba ya Zanzibar na kwa hiyo wataendelea na shughuli za Serikali kama kawaida.
Alidai
kuwa kazi ya uandikishaji wapigakura kwenye Wilaya ya Magharibi, Unguja
imetawaliwa na vitisho na kwamba watu wasiojulikana wamekuwa wakionekana
wakiwa na silaha za moto na kujifunika vitambaa usoni mithili ya
maninja na wengine kuvaa vinyago.
“Katika
maisha yangu sijawahi kuona askari anayekwenda kulinda akificha uso na
huu ni mkasa mpya duniani. Huwezi kumlinda raia kwa silaha za moto
wakati yeye hana chochote zaidi ya mikono yake,” alisema Duni.
Naibu
katibu mkuu wa CUF, Nassor Ahmed Mazrui alisema kuna vijana wamekwama
kuandikishwa na kuitaka Serikali kuondoa urasimu katika upatikanaji wa
vitambulisho vya ukazi.Alisema amechunguza na kubaini kuwa kuna vijana
walio na umri chini ya miaka 18 ambao wanaandikishwa kwenye kambi tatu
za jeshi ambazo hakuzitaja na baadaye kupewa vitambulisho ili
waandikishwe katika Daftari la Wapigakura.
Taarifa ya SMZ
Taarifa
iliyotolewa na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais, Mohamed
Aboud inasema hatua ya mawaziri kutoka ndani ya chombo hicho inakwenda
kinyume na kiapo cha kulinda na kutetea Katiba ya Zanzibar na kimeitia
doa SUK.
Alisema
haikuwa muafaka kususia kupitisha Bajeti Kuu ya serikali wakati
walishiriki katika kupanga na kuitayarisha kwenye vikao vya Baraza la
Mawaziri na kitendo hicho ni kwenda kinyume katika uwajibikaji wa
pamoja. “Lengo lao kubwa ni bajeti ishindwe kupita ili serikali ishindwe
kutoa huduma kwa wananchi. Bahati nzuri bajeti imepita lakini sisi kama
viongozi tusichanganye siasa na utekelezaji wa shughuli za serikali
tutairudisha nyuma Zanzibar na kuwaingiza wananchi katika matatizo,”
alisema.
Alisema
uandikishaji wapigakura na usajili wa vitambulisho vya Mzanzibari
hufanyika kwa kuzingatia sheria na katiba kama kuna kasoro walitakiwa
kuziwasilisha katika mamlaka zinazohusika.
Alisema
malalamiko yanayotolewa hayana msingi wala nguvu ya hoja kwa sababu Tume
ya Uchaguzi (ZEC)inaongozwa na makamishina kutoka vyama vya siasa,
ambavyo ni pamoja na CCM na CUF na hakuna malalamiko yaliyowahi
kutolewa.
Waliosalia wawananga
Akichangia
hoja ya bajeti, waziri wa zamani na mwakilishi wa jimbo la Kwamtipura,
Hamza Hassan Juma aliiomba Serikali iongeze muda wa siku tano apate
nafasi ya kuwasilisha hoja binafsi ili wananchi waulizwe kama bado
wanataka kuendelea na SUK au warudi kwenye mfumo wa zamani.
Alisema
kitendo kilichofanywa na mawaziri kususia shughuli za Serikali ndani ya
Baraza ni uvunjaji wa katiba ya Zanzibar ya mwaka 1984 ambayo waliapa
kuilinda na kuitetea wakiwa viongozi wakuu wa Serikali.
Alisema
kwamba kwa kuwa wao ni mawaziri na wamegoma kufanya kazi, wanapaswa
kukabidhi magari ya Serikali na kumtaka Rais wa Zanzibar kutumia mamlaka
aliyopewa kikatiba kuchukulia hatua suala hilo.
“Hata
kama rais atawaacha, katiba tayari imewafukuza na sasa wanapaswa waache
magari ya Serikali na wakafanye kazi nyingine Mtendeni. Haiwezekani
wanakula sambusa, keki Ikulu baadaye wanapinga kazi za serikali kinyume
na viapo vyao,” alisema Hamza huku akishangiliwa na wajumbe waliosalia.
Alisema
lengo la kuundwa SUK ilikuwa ni kujenga umoja, kuondoa chuki na ndio
maana Rais aliyepita, Amani Abeid Karume aliipigania SUK kama njia ya
kurejesha amani na utulivu kwa wananchi wa Zanzibar.“Wenzetu wameamua
kuanzisha vurugu lazima tukae upya tuangalie kama kuna sababu ya
kuendelea na mfumo wa serikali ya pamoja. Yanayotokea sasa ni kinyume na
malengo ya kuletwa kwa mfumo wa serikali ya pamoja,” alisema.
Wajumbe
wengine waliochangia ni Waziri wa Elimu na Mfunzo ya Amali, Ali Juma
Shamhuna aliyesema mawaziri hao walisusia kikao bila ya kuwa na hoja ya
msingi.
“Mheshimiwa
Spika, wenzetu waliahidi kuondoa matatizo mbalimbali kwa bajeti zao za
mwaka huu, ikiwamo suala la ukosefu wa taa kwenye Uwanja wa Ndege wa
Pemba, leo wanasusia kupitisha bajeti kuu, wanataka maendeleo au
hawataki?” alihoji.
Taarifa ya CUF
Baadaye
CUF ilitoa taarifa kwa vyombo vya habari ikiilaumu ZEC kwa kuendelea
kuandikisha watu kwenye Daftari la Wapigakura licha ya kuwapo kasoro
nyingi.
Mwakilishi
wa Jimbo la Mji Mkongwe, Ismail Jussa Ladhu alieleza katika taarifa
hiyo kuwa uandikishaji umekumbwa na vurugu zilizotokana na kutumika kwa
vyombo vya dola vinavyolazimisha watu wasio na sifa kuandikishwa.
Alisema:
“CUF inaeleza kwamba vitambulisho 109 vilikataliwa kutambuliwa na
mashine za BVR, lakini masheha na vikosi vya Serikali walilazimisha watu
kuandikishwa.
“Tume ya
Uchaguzi ilikataa kutoa idadi ya askari waliohamia kutoka maeneo
mengine, huku watu wakipigwa na kukamatwa, wakiwamo waliokwenda katika
vituo vya polisi kuwawekea dhamana wenzao waliokamatwa,” inasema taarifa
hiyo.CHANZO:MWANANCHI
No comments:
Post a Comment