Siku moja baada ya kifo cha dada wa bilionea Erasto Msuya, Aneth imebainika kuwa msaidizi wa ndani aliondoka saa sita mchana kwa kuacha funguo nyumba ya jirani.
Akizungumza nyumbani kwa dada wa marehemu, Mbezi Juu, mama mdogo wa marehemu Lilian Benjamin alisema msaidizi huyo alimpigia simu bosi wake mchana na kumwambia anaondoka na hataendelea na kazi.
Alisema marehemu alilazimika kuomba ruhusa mapema kazini ili arudi nyumbani kwake Kibada lakini ilimlazimu kukaa nje ya nyumba kwa saa mbili baada ya kufika saa tisa alasiri na kukuta mlango umefungwa.
Mama huyo alisema baada ya kusubiri kwa muda aliwauliza majirani wakamweleza kuwa walipelekewa funguo na mwanafunzi wasiyemfahamu akadai kuwa alipewa na dada mmoja aliyemuelekeza aipeleke nyumba hiyo.
Haifahamiki mpaka sasa mahali alipo mfanyakazi huyo anayedaiwa kuwa mwenyeji wa Arusha.
Dada mkubwa wa marehemu, Happy Msuya alisema marehemu aliwaeleza mambo hayo baada ya kupigiwa simu na msichana huyo wa kazi.
Dada mwingine wa marehemu ambaye ni wa nne kuzaliwa kati ya watoto saba wa Elisaria Msuya, Ester, alisema wauaji hao hawakuwa na nia ya kuiba, bali ni kuua kwa sababu hawakuchukua kitu chochote zaidi ya televisheni ambayo nayo waliitupa mbali na nyumbani.
Ester alisema mara ya mwisho kuonana na marehemu ilikuwa Mei saba walipokutana benki na mazungumzo yao yalihusu hali ngumu ya maisha. Alisema hakuwahi kumwambia kama ana ugomvi na mtu kwa sababu alikuwa mpole na msiri.
Akielezea tukio hilo alisema inaonekana kulikuwa na purukushani kubwa chumbani kwa sababu besela la kitanda lilikuwa limevunjika na neti ilikuwa imetoka, huku nyaraka zikiwa zimepekuliwa na kusambazwa karibu kila kona ya chumba.
“Walikuja kuua, kuna kitu walikuwa wanatafuta katika nyaraka pia, ooh... Aneth umekufa kinyama, umechinjwa kama mnyama,” Ester alishindwa kuendelea na kuanza kulia na baadaye kidogo alisema wauaji walimkata marehemu koromeo lakini hawakutenganisha kichwa na kiwiliwili.
Simulizi ya mtoto
Mtoto wa marehemu mwenye umri wa miaka minne ambaye alikuwa akiishi na mama yake alisema: “Walikuja watu watano weusi usoni, wakanifanya na kitu shii usoni, nikalala kwenye kiti mbu wameniuma hadi niliposikia gari la shule likiita pipii, nikaamka na nikamuamsha mama anivalishe nguo za shule lakini akakataa kuamka, ”alisema mtoto huyo na kuongeza.
“Nikavaa mwenyewe nguo za shule na nikamwambia mama nitaendaje shule huku sijafanya “Home work” lakini mama hakujibu, mbu walining’ata pale kwenye kochi nilipolala, nikatoka nje nikakuta gari limeshaondoka, nikaenda kwa mama Salum,”alisema.
Alisema alienda huko akale kwa sababu njaa ilikuwa inamuuma hakula jana yake baada ya ‘wageni’ hao kuja na yeye kulala.
Alieleza kuwa alipowaambia mama yake hamjibu amelala tu alirudi na dada ambaye amemsahau jina kutoka hapo kwa mama Salum ambaye alipofika nyumbani kwao na alipomuona mama yake alianza kupiga kelele.
Ester alisema mwili wa marehemu utasafirishwa Jumatatu ijayo kuelekea kijijini kwao Kairo, Simanjiro mkoani Manyara.
Mtu wa karibu na familia ambaye hakutaka jina lake litajwe alisema mbali ya kaka yao Erasto kuuawa kwa risasi, dada yao Ester akiwa na mumewe katika Baa ya Hongera, Dar es Salaam alipigwa risasi na kunusurika kufa.
No comments:
Post a Comment