Serikali
imeieleza Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu kwamba itafika na mashahidi
wasiozidi 10 katika kesi ya kutumia na kujihusisha na dawa za kulevya
inayomkabili mfanyabiashara, Yussuf Manji.
Hayo
yameelezwa na Wakili wa Serikali Mkuu, Timony Vitalis mbele ya Hakimu
Mfawidhi, Cyprian Mkeha baada ya kumsomea Manji maelezo ya awali (Ph)
ambapo katika maelezo hayo, Vitalis amedai mshtakiwa ni mkazi wa Sea
view DSM, pia ni mfanyabiashara anayetuhumiwa kujihusisha na kutumia
dawa za kulevya.
Amedai
kuwa alikamatwa February 2, 2017 kisha akapelekwa kituo cha Polisi
ambapo alichukuliwa hadi nyumbani kwake na kupekuliwa na baada ya
kupekuliwa alipelekwa kwa Mkemia Mkuu wa Serikali na kuchukuliwa haja
ndogo (Mkojo) ambao ulipimwa na kukutwa na dawa za kulevya aina ya
Benzodiazepine.
Baada
ya kusomewa maelezo hayo, Manji alikubali wasifu wake kwamba ni
mfanyabiashara, makazi na jina lake licha ya kudai limekosewa ila
usahihi ni Yusuf Manji huku akikana maelezo mengine.
Aidha,
wakili Vitalis ameieleza Mahakama kwamba wanaomba kupangiwa tarehe kwa
ajili ya kesi hiyo kuanza kusikilizwa, pia wanatarajia kuwa na mashahidi
wasiozidi 10 hivyo Hakimu Mkeha ameahirisha kesi hiyo hadi August 22,
23, na 24, 2017 kwa ajili ya kusililizwa mfululizo.
No comments:
Post a Comment