Ujumbe
wa watu zaidi ya 300 unaomwakilisha Mfalme wa Oman, Shekh Sultan Qabous
Bin Said umewasili visiwani Zanzibar leo Alhamisi asubuhi kwa kutumia
meli yenye jina la Fulk Al Salamah ambayo hutumiwa na mfalme huyo.
Ujumbe
huo wa Serikali ya Oman umewasili katika Bandari Kuu ya Malindi mjini
hapa majira ya saa tatu na nusu za asubuhi ikitokea nchini Oman.
Katika
mapokezi ya ujumbe huo viongozi wa Serikali ya Zanzibar walihudhuria
akiwamo Waziri wa Habari, Utalii, Utamaduni na Michezo, Rashid Ali Juma,
Waziri Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais, Mohamed Aboud Mohamed, Waziri
wa Maji, Nishati, Ardhi na Mazingira, Salama Aboud Talib na Wazir wa
Biashara na Masoko, Amina Salum Ali.
Kwa
upande wa ujumbe huo wa mfalme uliongozwa na Waziri wa Mafuta na Gesi
wa Oman, Mohamed Al-ramh ambapo lengo kuu la kufika Zanzibar ni
kusambaza amani na upendo ikiwa ni hatua ya kufikisha ulimwenguni kote.
Akizungumza
katika mapokezi hayo Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamo wa Pili wa Rais,
Mohamed Aboud Mohamed amesema ni faraja kubwa kwa Zanzibar kupata ugeni
huo wa heshima.
Amesema
ugeni huo ni ishara njema ya kufungua ukurasa mpya wa ushirikiano baina
ya nchi hizo mbili ambazo zinaonekana kuwa na udugu wa kihistoria kwa
miaka mingi.
‘’Ishara
hii ni njema na tunaifurahia kwa moyo wote na kesho tutakuwa na
mazungumzo rasmi na ugeni huo ambapo tunataraji mambo mbalimbali
tutayajadili na baadaye kutoa taarifa rasmi ya mazungumzo yetu,”
amesema Aboud.
Hata
hivyo amesema ujumbe huo pia utapa nafasi ya kutembelea maeneo
mbalimbali ya kihistoria, ofisi za Serikali lengo ni kubadilishana
mawazo juu ya ukuaji wa uchumi.
No comments:
Post a Comment