Monday 1 April 2013

UCHINJAJI NYAMA WALETA MTAFARUKU TUNDUMA

SAKATA la uchinjaji kati ya Waislamu na Wakristo limeingia katika sura mpya baada ya waumini wa madhehebu hayo katika Mji wa Tunduma wilaya ya Momba mkoani Mbeya, leo kuamua kujichinjia wenyewe katika machinjio moja ya serikali.

Kwa mujibu wa mashuhuda walioshuhudia tukio hilo wameeleza kuwa asubuhi ya siku ya Pasaka Machi 31, zilichinjwa jumla ya ng’ombe 40 ambapo inadaiwa kuwa kati ya hizo ng’ombe 3 walikuwa wa waislamu na 37 walikuwa wa wakristo.

Silanda Barton ni mmoja wa mashuhuda hao alisema kuwa, baada ya uchinjaji huo kufanyika alifika mkaguzi wa nyama ambapo alishitushwa na hali ambayo haikuwa ya kawaida ndipo alipokagua nyama ya ng’ombe watatu waliochinjwa na waislamu na kuamua kuacha hali ambayo iliwafanya wengine kuamua kuzuia nyama hiyo isiuzwe.

Barton alisema hata hivyo wateja waliofika buchani siku ya leo ili kujipatia kitoweo hicho walifanya jitihada za kumuomba afisa mifugo huyo ili aweze kukubali kupima nyama nao wajipatie kitoweo.

Hata hivyo Afisa Mifugo huyo ambaye ametambulika kwa jina moja la Tarimo alikubali kufanya ukaguzi na ndipo nyama ikaanza kuuzwa mchana.

Alisema Wakati mzozo huo ukiendelea  kundi moja la vijana (Vibaka) waliingilia kati kwa lengo la kuukuza ili patokee vurugu ambazo zingewanufaisha kwa kupora mali.

Aidha kutokana na hali kutokuwa washari jeshi la polisi kikosi cha kuzuia ghasia (FFU) kilifika katika eneo hilo ili kuimarisha ulinzi zaidi.

Mkuu wa wilaya ya Momba Abihudi Saideya alipotafutwa kupitia simu yake ya mkononi hakuweza kupokea na alipopigiwa dereva wake alidai yupo katika eneo la tukio kujaribu kuweka mambo sawa.

Vurugu katika mji wa Tunduma zimekuwa zikijitokeza mara kwa mara ambapo lipo kundi la vijana ambalo limekuwa likishabikia mambo ili kuyakuza kwa lengo la iwapo itatokea vurugu lipata nafasi ya kupora mali.


 

No comments: