WANACHAMA wa Klabu ya Yanga
wamehamasishwa kufungua akaunti katika Benki ya Posta ili kuchangia timu yao na
kulipa ada bila usumbufu.
Hayo yalisemwa jana katika Mkutano
wa Meneja wa Benki ya Posta Mkoa wa Mbeya na viongozi wa Matawi uliofanyika
katika ukumbi wa Coffee Garden uliopo jijini Mbeya wenye lengo la kuwahimisha
kuwahamasisha mashabiki wao kufungua hizo akaunti.
Meneja wa Benki hiyo Mkoa wa Mbeya,
Humphrey Julius, alisema mradi huo ni mpya ambao utamwezesha mwanachama
kuchangia klabu kila anapotumia huduma ya benki.
Alisema Benki ya Posta iligundua kuwa
Klabu za Simba na Yanga zinawapenzi wengi ambao hawajui jinsi ya kuchangia timu
zao ambapo ilibuni akaunti maalumu ambayo shabiki atapewa kadi itakayotumika
kupata huduma za kifedha kama kawaida ambapo mchango wake huingia moja kwa moja
kwenye klabu.
Alisema mwanachama na mpenzi wa klabu
hiyo atakuwa akikatwa shilingi 250 kwa wiki kwenye akaunti yake ambazo zitakuwa
zikiingia moja kwa moja kwenye akaunti ya klabu hivyo kuzinufaisha na kumfanya
mwanachama kuwa hai.
Alisema utaratibu huo utasaidia klabu
kuacha utegemezi wa kuomba misaada kwa wafadhili na watu wasiokuwa na mapenzi
na tumi bali itakuwa inapata michango na ada kutoka kwa wanachama wao moja kwa
moja.
Nao baadhi ya Wanachama na wapenzi wa
klabu ya Yanga Mkoa wa Mbeya wameulalamikia uongozi wa juu wa timu hiyo kwa
kushindwa kutoa elimu kwa wanachama wake kuhusu mkataba walioingia na Benki ya
Posta (TPB).
Wanachama hao ambao ni viongozi wa
matawi ya Yanga Mkoa wa Mbeya ambao hawakutaka majina yao kuandikwa walisema
kinachofanyika ni benki kufanya biashara kwa kuwahamasisha kufungua akaunti
bila kuwaambia manufaa anayopata mtu mmoja mmoja.
Walisema utaratibu uliokuwepo awali
ulikuwa kila mwanachama anachangia shilingi 1000 kwa mwezi ambapo kulikuwa na
akaunti maalumu ya Benki ambayo kila mwanachama na mpenzi wa klabu alikuwa
analipia huko.
Mwisho.
|
No comments:
Post a Comment