Mbeya. Jiji la Mbeya kwa kushirikiana na kampuni moja
inadaiwa kufanya utapeli kwa vijana zaidi ya 900 na kuvuna mamilioni ya fedha
za vijana hao kwa madai ya kupatiwa mafunzo ya komputa.
Takwimu zilizopatikana hadi jana ni
kwamba Jiji hilo kwa kushirikiana na Kampuni iliyojulikana kwa jina KEAR
Computer Training Centre, wamejipatia kiasi cha zaidi ya Sh46 milioni kutoka
kwa vijana hao.
Mbali ya vijana hao kutapeliwa,
ilielezwa kwamba nao utapeli huo ulilenga pia kwenye sekondari tisa na shule za
msingi 22 za Serikali jijijini hapa ambapo wanafunzi waliagizwa kutoa Sh1,000
kila mmoja kwa ajili ya picha za wanafunzi watakaoingia kwenye mpango huo.
Ofisa Elimu ya Sekondari, Lydia
Herbert alikiri kuwa kwa tukio hilo akisema ndiye aliyeshiriki kuzungumza na
mwenye kampuni ya Kear aliyetajwa kwa jina la Uttu Kingwande na kwamba aliahidi
kuwapatia mafunzo walimu wawili wawili
kutoka kila shule.
Lydia alisema Kigwande alifika
ofisi ya jiji akiwa na nyaraka zilizoonyesha kwamba aliwahi kufanya kazi Dodoma
na Temeke Dar es Salaam na pia alifanya mazungumzo na viongozi mbalimbali ya
jiji akiwahakikishia kutoa misaada ya kompyuta.
Wakisimulia mkasa huo kwa niaba ya
wenzao wanafunzi 10,( majina yanahifadhiwa) walisema mapema Mei mwaka huu viongozi wa Jiji wakiongozwa na
Naibu Meya wa Jiji hilo, Chifoda Fungo na watendaji wa Serikali za Mitaa
walifika katika Kata zote wakiwa wameambatana na mtu aliyetajwa kuwa ni jina la Uttu Kingwande kuwa ni mkurugenzi wa
Kampuni hiyo huku wakiwa na nyaraka zote
za kuitambulisha kampuni hiyo.
“Tuliambiwa kuwa watakaokuwa tayari watume maombi kupitia kwa wenyeviti na watendaji wa
Serikali za Mitaa kwa ajili ya kujiunga na chuo hicho ambacho kituo chake
kilikuwa katika Shule ya Sekondari ya Mbeya. Na sisi tulipoona viongozi wa
Serikali ndio wanaopita na kutuhamasisha kitu hicho huku wakiwa na nyaraka zote
hatukuwa na shaka yoyote, tukajitokeza wanafunzi zaidi ya 900 na tulipofika
pale tukaambiwa mafunzo hayo ni bure isipokuwa kila mwanafunzi atachangia
Sh40,000 kwa ajili ya cheti na usajili wa kuhitimu mafunzo hayo na wote tulitoa”
Walisema wanafunzi 150 kati yao walichanga
Sh70,000 zingine kila mmoja ili kupata kompyuta mpakato na baada ya hapo Mkurugenzi
huyo aliondoka kwa madai kuwa anafuata kompyuta hizo lakini mpaka sasa
hajarudi.
Tumesikia mhasibu wake Rehema Ramadhani amekamatwa hivyo tumeshtuka na tunapojaribu
kufuatilia hatuoni mwanga’’ walisema.
Akizungumza kwa njia ya simu, Naibu Meya wa jiji hilo,
Chifoda Fungo ambaye pia ni diwani wa Kata ya Uyole Kati, alikiri kuutambua
mradi huo na kwamba yeye alifanya kazi kawenye kata yake pekee na haamini
kwamba ni utapeli.
“Sio kweli kwamba nilizunguka kata zote, mimi
nilipita kuwahamasisha wananchi wa kata yangu na baada ya kuona jambo hilo la
kheri nikawahidi kuwachangia kiasi fulani cha fedha vijana watakaotoka kwenye kata
yangu na si vingenevyo” alisema Fungo.
Naye Mkurugenzi wa Jiji Mussa
Zungiza akiwa mkoani Tanga kikazi alikiri kuutambua mpango huo na kwamba
mchakato ulivyokuja haukuonekana kuwa wa utapeli, lakini sasa hali imegeuka na
kutaka kulichafua jiji.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mbeya, Ahmed
Msangi alipoulizwa juu ya sakata hilo alikiri kumhoji ofisa wa kampuni hiyona
kwamba uchunguzi unaendelea.
No comments:
Post a Comment