Wednesday 6 May 2015

KUMEKUCHA CCM

  • Wanaotaka urais kujulikana Juni
  • Wakiuka sheria kukiona
  • Mbwembwe marufuku
CHAMA Cha Mapinduzi (CCM) kinatarajiwa kuanza kutoa fomu kwa watu wanaotaka kuwania urais kupitia chama hicho mwanzoni mwa mwezi ujao, Raia Mwema limeambiwa.
Hata hivyo, chama hicho kinatarajia kubadilisha baadhi ya taratibu za mchakato mzima wa uchukuaji wa fomu hizo tofauti na ilivyokuwa wakati wa kutafuta mgombea wa chama hicho mwaka 2015.
Vyanzo vya kuaminika vya gazeti hili vimeeleza kwamba wanaotaka kuwania urais kupitia CCM wataanza kuchukua fomu zao mwanzoni mwa mwezi ujao kupitia utaratibu maalumu utakaotangazwa.
"Chama kitaruhusu wagombea kuchukua fomu katika wiki ya kwanza ya mwezi Juni mwaka huu kupitia utaratibu maalumu utakaotangazwa na chama wakati ukifika," kilieleza chanzo hicho kilicho karibu na uongozi wa juu wa CCM.
Tofauti na katika chaguzi za mwaka 1995 na 2005, safari hii CCM inaendesha mchakato wake wa kutafuta wagombea katika hali ya usiri mkubwa, huku ikielezwa kwamba chama hicho hakitaki kufanya makosa yatakayonufaisha vyama vya upinzani.(P.T)
Gazeti hili limeambiwa kwamba hivi sasa, CCM kinaandaa taratibu na kanuni zitakazotumika katika mchakato huo na kwenye ngazi za ubunge na udiwani ambazo katika baadhi ya mambo ni tofauti na zile zilizotumika mwaka 2005.
Kwa mfano, Raia Mwema limeambiwa kwamba huenda chama kikaangalia upya utaratibu wa kutafuta wadhamini mikoani tofauti na ule uliotumika mwaka 2005.
Mwaka 2005, waliokuwa wasaka urais kupitia CCM walilazimika kutafuta wadhamini katika mikoa tofauti ya Tanzania Bara na Zanzibar ili kuonyesha kuwa wanaungwa mkono na wanachama wa mikoa mbalimbali na pande zote mbili za Muungano.
Itakumbukwa kwamba wakati huo, aliyekuwa mgombea mwenye nguvu ndani ya CCM, John Cigweyemisi Malecela, alizunguka mikoani kwa ndege ya kukodi na kumaliza zoezi hilo ndani ya wiki moja.
"Watu wengi hawafahamu lakini wakati tulipokuwa na mchakato kama huu mwaka 1995, haikuwa lazima kwa wagombea kuzunguka mikoani kutafuta wadhamini. Tuliokuwa ndani ya chama wakati huo tukishuhudia kila kitu hili halikuwepo.
"Lakini chama kikatumia utaratibu huo wa kutafuta wadhamini mwaka 2005 ambao haukuwepo huko nyuma. Hivyo, mwaka huu, chama kinaweza kuona kuwa ni busara kutoendelea na utaratibu kama huo,"
"Chama ni chombo kilicho dynamic (kinachobadilika). Hatuwezi tukaacha CCM iwe static (bwete). Kwa mfano, kama mwaka 1995 tulikataza watu wasiende mikoani ili kuzuia wasitoe rushwa, mwaka huu hali imebadilika. Si lazima mtu akutane na mtu ndiyo atoe rushwa. "Akiwa na simu yake ya mkononi anaweza kumpa rushwa yeyote amtakaye, popote pale alipo hapa nchini. Ndiyo maana chama hakiwezi kuwa na mawazo mgando. Ni lazima kanuni na taratibu zake ziakisi wakati husika," kilisema chanzo hicho cha Raia Mwema.
Raia Mwema limeambiwa kwamba katika uchaguzi wa mwaka huu, wana CCM wanatamani kuona kuwa watu wote wanaojitokeza kutaka kuwania nafasi hiyo wanapata fursa sawa ya kuendesha shughuli zao.
"Kuna wagombea watakuwa na uwezo wa kuwa na ndege za kukodi na wengine hawatakuwa nao. Kuna wagombea wanaweza kuwa na msafara wa magari 100 na wengine mawili tu.
"Kuna wagombea wana nafasi kubwa serikalini ambazo zinawapasa kusindikizwa na ving'ora na wana walinzi. Mwaka 2005, kama unakumbuka, aliyekuwa Waziri Mkuu, Frederick Sumaye, alienda kuchukua fomu bila msafara. Tunataka hali iwe hivyo pia safari hii.
"Mwaka huu, sidhani kama chama kitakubali wagombea wengine waonekane wana faida kuliko wenzao. Lengo ni kwamba, kila mgombea apate fursa sawia ya kukutana na wanachama na kueleza yale aliyokusudia kuyafanya endapo chama kitampitisha," mmoja wa wagombea aliyewania nafasi hiyo mwaka 2005 na ambaye anatajwa kutaka kuwania tena nafasi hiyo mwaka huu aliliambia gazeti hili juzi Jumatatu.
Ubunge
Katika hatua nyingine, gazeti hili linafahamu kwamba kuna uwezekano mkubwa chama hicho kikabadili utaratibu wake wa kupata wagombea wa nafasi ya ubunge kulinganisha na ule uliotumika mwaka 2005.
Wapo wana CCM wanaoamini kwamba chama chao kilipoteza baadhi ya viti vya ubunge mwaka 2005 kutokana na utaratibu mbovu wa kutafuta wabunge kupitia mtindo wa kura ya maoni.
"Unakuta kwenye jimbo moja chama kina watu 20 wanaotafuta nafasi moja tu ya ubunge. Utaratibu uliotumika mwaka 2005 ulikuwa kwamba wote hao wanakwenda kupigiwa kura na wana CCM kwenye majimbo yao jambo ambalo lilileta matatizo mengi.
"Kuna watu ndani ya chama wanaamini kwamba inatakiwa vyombo vya chama vifanye kazi yake kiasi kwamba majina yanayokwenda kwenye kura ya maoni yasizidi matatu. Na hao watatu ni lazima wawe wale ambao wamefuata taratibu zote za chama.
"Hili litazuia watu kutoa rushwa mapema na hovyo hovyo. Maana, kama mko watu 20, nani atatoa rushwa wakati akijua wanatakiwa watu watatu tu na tena waliofuata taratibu zote?" alisema mmoja wa waliokuwa viongozi wa CCM Mkoa wa Dar es Salaam mwanzoni mwa miaka ya 2000.
Akizungumza na Raia Mwema kuhusu kuthibitisha kuanza kwa mchakato huo mwezi ujao, Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Nape Nnauye, alisema chama kitatoa taarifa kuhusu jambo hilo wakati ukifika.
"Nimewahi kusema huko nyuma na sijui kama mlinisikia kuwa CCM haitawahi wala kuchelewa kwenye suala la uchaguzi wa mwaka huu. Wakati ambao tutaamua kufanya mambo yetu utakuwa ndiyo wakati sahihi na wenyewe.
"Haya mambo yanakwenda kwa pamoja. Unaweza kufanya uamuzi sahihi ikiwa si kwa wakati, unaharibu. Uamuzi sahihi unaendana na wakati sahihi. Katika wakati sahihi ukifika, tutafanya uamuzi sahihi," alisema Nape.
Kuhusu madai kwamba safari hii CCM imetawaliwa na usiri mkubwa katika mchakato mzima wa uchaguzi, Nape alisema suala hilo si la kweli kwani linavumishwa na watu wasiojua utendaji wa chama hicho.
Alisema mara nyingi ratiba ya uchaguzi ndani ya CCM hupangwa kuendana na ile inayotolewa na Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) ambayo hadi sasa haipo.
Ingawa hadi sasa chama hakijafungua rasmi milango kwa wagombea wake kujitangaza na kupiga kampeni za waziwazi, tayari baadhi ya majina yamekuwa yakitajwa mara kwa mara kuwa yataingia kwenye kinyang'anyiro cha kumrithi Rais Jakaya Kikwete.
Miongoni mwa majina yanayotajwa kutoka ndani ya CCM ni Edward Lowassa, Bernard Membe, Mizengo Pinda, Profesa Mark Mwandosya, January Makamba, Frederick Sumaye, Steven Wasira, Dk. Asha Rose Migiro, Makongoro Nyerere na Dk. Hamis Kigwangala.

No comments: