SERIKALI imefanikiwa kumaliza sintofahamu ilikuwepo
baina ya wakulima na wanunuzi wa tumbaku mkoani Tabora juu ya uwepo wa tani
3,700 zilizokosa soko.
Tani 3,700 zilikuwa zimekosa wanunuzi kwa sababu
hazikuwa na mkataba kati ya wakulima na wanunuzi na hivyo kuhitaji utatuzi wa
haraka wa Serikali ili kuinusuru tumbaku hiyo.
“Tumefanikiwa kuongea nao na tutauza zile tani
3,700 kwa wanunuzi,” alisema Waziri Mkuu Kassim Majaliwa na kuamsha shangwe
ukumbi mzima.
Waziri Mkuu alitoa ahadi hiyo jana jioni (Jumatano,
Agosti 9, 2017) wakati akizungumza na wadau wa zao la tumbaku zaidi ya 600
wakiwemo wabunge, viongozi wa dini, chama na Serikali kwenye mkutano
uliofanyika katika ukumbi wa Isike-Mwanakiyungi, mjini Tabora.
Aliwashukuru wanunuzi kwa kukubali kumaliza tatizo
hilo kwani litaleta ari mpya kwa wakulima na kuwafanya wajipange vizuri kwa
msimu ujao. “Makampuni ya ununuzi yatapita kwenye maeneo yenu, WETCU
watafuatilia na tumekubaliana nao kuwa tutafanya kazi pamoja,” alisema Waziri
Mkuu.
Kufuatia sintofahamu hiyo, wiki iliyopita, wakazi
wa mkoa huo waliomuomba Mheshimiwa Rais, Dkt. John Pombe Magufuli aingile kati
ili kuwanusuru na adha ya zao hilo kukosa soko. Naye akawaahidi wananchi hao
kwamba suala hilo atalikamilisha Waziri Mkuu.
Mapema, Mkuu wa Mkoa wa Tabora, Bw.
Aggrey Mwanri wakati akiwasilisha muhtasari wa taarifa ya mkoa huo alisema
katika masoko ya tumbaku yanayoendelea, kuna tatizo la tumbaku kukosa wanunuzi kwani hapakuwa na mkataba kati ya
wakulima na wanunuzi.
“Tumbaku inayofikia kilo milioni 3.7 kwa sehemu
kubwa ililimwa kwa ufadhili wa WETCU Ltd,
kwa fedha ambazo zilikuwa ziende APEX. WETCU walinunua pembejeo na kuwapa
wakulima waliokuwa chini ya vyama sinzia, na sasa haina wanunuzi. Tunaomba
ulisemee hilo ili tupate ufumbuzi wa suala hili,” alisema.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Wabunge wa Mkoa wa Tabora ambaye pia ni mbunge wa Urambo,
Mheshimiwa Margareth Sitta aliiomba Serikali ikubali kuliangalia suala hilo la
tani za ziada 3,700 kwani wakulima wamejaza tumbaku majumbani mwao na kwenye
maghala.
“Wakulima wetu wanahitaji kuuza hii tumbaku ili
wapate fedha za kuanzia msimu ujao wa kilimo. Lakini pia tunaomba liangaliwe
suala la upangaji madaraja ya tumbaku, wasaidiwe kukabili bei isiyotabirika na
kutatua ukosefu wa soko la uhakika,” alisema Mama Sitta.
No comments:
Post a Comment