Thursday, 10 August 2017

WAZIRI MKUU APIGA MARUFUKU VIONGOZI KUFANYA BIASHARA YA PEMBEJEO KAMA HAWANA MASHAMBA.



WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amepiga marufuku viongozi wa Serikali kufanya biashara ya pembejeo na vishada kama hawana mashamba ya tumbaku.

“Kuna baadhi ya viongozi wa Serikali hapa mkoani wamejiingiza kwenye biashara ya vishada na uuzaji wa pembejeo. Hii ni dosari. Hatutaruhusu hili hata kidogo,” alisema.

Waziri Mkuu alitoa onyo hilo jana jioni (Jumatano, Agosti 9, 2017) wakati akizungumza na wadau wa zao la tumbaku zaidi ya 600 wakiwemo wabunge, viongozi wa dini, chama na Serikali kwenye mkutano uliofanyika katika ukumbi wa Isike-Mwanakiyungi, mjini Tabora.

Alisema: “Kiongozi wa Serikali ni lazima uwe shamba na ulilime kisasa ili liwe ni shamba darasa kwa wakulima walio jirani nawe. Usifanye biashara ya pembejeo kana huna shamba. Nanyi viongozi wa AMCOS msikubali kuuza vishada vya viongozi wa Serikali, tukikukamata, utaenda jela.”

Alisema endapo viongozi wataamua kulima mashamba ya zao hilo, watalazimika kujiunga na vyama vya msingi (AMCOS) vya kwenye maeneo yao ili waweze kuuza kupitia huko kutokana na agizo la Serikali linalokataza makampuni kununua tumbaku bila kupitia kwenye vyama vya msingi.
 
Aprili 15, mwaka huu, akiwa katika ziara ya siku moja mkoani Tabora, Waziri Mkuu aliagiza wakulima wa kujitegemea (Indepenent Farmers) na wale wa kwenye vikundi (Associations) wote wauzie tumbaku yao kupitia kwenye vyama vya ushirika ili kuzuia utoroshaji wa zao hilo na wakulima wasio na madeni kulazimika kuwalipia wenzao.
IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,
ALHAMISI, AGOSTI 10, 2017.

No comments: