Monday, 4 May 2015

Shuka yamuua mwendesha pikipiki Kiteto




MKAZI wa Kijiji cha Ndeleta kilichopo wilayani Kiteto, Mkoa wa Manyara, Saria Kidali (47), amefariki dunia baada ya kunyongwa na shuka alilokuwa amejifunika wakati akiendesha pikipiki.

Tukio hilo la aina yake lilitokea jana asubuhi wakati Kidali alipokuwa akitoka shambani kwake Nadosoiti.
 
Kabla ya kifo hicho, shuka ya mwendesha pikipiki huyo ilinasa kwenye tairi ya nyuma na shuka hiyo kumbana shingo Kidali hadi alipopoteza maisha baada ya kudondoka chini.

Kamanda wa Polisi, Mkoa wa Manyara, Christopher Fuime, alithibitisha kutokea kwa tukio hilo na kuitaja pikipiki iliyomuua Kidali kuwa ni aina ya Toyo yenye namba za usajili T613 BEB.

“Pikipiki hiyo inasemekana ni mali ya marehemu na taarifa za awali zinaonyesha chanzo cha kifo hicho ni shuka alilokuwa amevaa kwani lilijizungusha kwenye tairi na kumnyonga shingo,” alisema Kamanda Fuime.

Pamoja na hayo, alitoa wito kwa waendesha pikipiki kuchukua tahadhari wakati wote ili kuepukana na ajali zinazoweza kuepukika.

Baadhi ya mashuhuda wa tukio hilo, waliitonya MPEKUZI kwamba, walipata taarifa za tukio hilo kutoka kwa abiria wa basi moja la abiria lililokuwa likitoka wilayani Kiteto kuelekea Arusha.

Mmoja wa mashuhuda hao aliyejitambulisha kwa jina la Lazaro Gidion, alisema marehemu Kidali hakukutwa na majeraha yoyote ingawa shingo yake ilikuwa imezungukwa na shuka.

Naye Mwenyekiti wa Kijiji cha Ndaleta lilikotokea tukio hilo, Ijumaa Bakari, aliwataka wananchi wa eneo hilo kutovaa shuka wakati wanaendesha pikipiki kwa kuwa zinaweza kuhatarisha maisha yao

No comments: