Monday, 4 May 2015

Upelelezi Kesi ya Gwajima Mbioni Kukamilika



UPELELEZI wa kesi inayomkabili Askofu wa Kanisa la Ufufuo na Uzima Mchungaji  Josephat Gwajima na wenzake watatu unadaiwa uko mbioni kukamilika.
 
Taarifa hiyo iliwasilishwa jana katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu na Wakili wa Serikali Mwandamizi, Shadrack Kimaro mbele ya Hakimu Mkazi Frank Moshi wakati kesi hiyo ilipotajwa.
 
Wakili huyo alidai kesi hizo zililetwa mahakamani hapo kwa ajili ya kutajwa na kwamba upelelezi wake upo mbioni kukamilika hivyo anaomba ziahirishwe waweze kukamilisha.
 
Hakimu alikubaliana na ombi hilo na kuahirisha kesi hizo hadi Juni 4 mwaka huu.
 
Washtakiwa wengine katika kesi hiyo ni Msaidizi wa askofu huyo,  Yekonia Bihagaze (39), mfanyabiashara George Mzava (43) na Mkazi wa Kimara Baruti Geofrey Milulu (31).
 
Katika kesi ya kwanza namba 85,Gwajima anadaiwa kwamba kati ya Machi 16 na 25 mwaka huu katika Viwanja vya Tanganyika Pekas alitoa lugha ya matusi dhidi ya Askofu wa Kanisa Katoliki Muwadhama Policapy Kardinaly Pengo.
 
Gwajima anadaiwa kumuita pengo kuwa ni mtoto, mpuuzi asiye na akili katika namna ya kwamba ingeleta uvunjifu wa amani.
 
Katika kesi ya pili namba 84 , Gwajima anakabiliwa na shtaka moja la kushindwa kuhifadhi silaha na risasi kinyume cha sheria ya uhifadhi wa siraha za moto.
 
Anadaiwa kwamba kati ya Machi 27 na 29 mwaka huu ndani ya jiji na Mkoa wa Dar es Salaam, alishindwa kuhifadhi silaha aina ya Beretta namba CAT 5802 ,risasi 3 za pisto na risasi 17 za Shortigan.
 
Shtaka la pili na la tatu linawakabili washtakiwa waliobaki ambao wanadaiwa kwamba Machi 29 mwaka huu katika Hospoitali ya TMJ Mikocheni ‘A’ walikutwa wakimiliki silaha na risasi hizo bila ruhusa kutoka mamlaka husika.

No comments: