Wednesday, 24 June 2015

CCM yaitaka serikali kuondoa muswada wa habari


Chama cha mapinduzi kimeitaka serikali kusikiliza ombi la wamiliki na wadau wa habari, kuondoa sheria ya haki ya kupata habari mpaka pale wadau wote watakapojadiliana na kukubaliana ndipo ikajadiliwe bungeni.
Nape Nnuye katika mkutano wa hadhara wilayani Misungwi
Kauli hiyo imetolewa na katibu wa NEC Itikadi na Uenezi wa CCM taifa, Nape Nnauye, wakati akihutubia wakazi wa Misungwi mkoani Mwanza kwenye mkutano wa hadhara, ambapo ameitaka serikali kuwasikiliza wananchi na wadau wa habari juu ya sheria hiyo na sheria nyingine ambazo zimekuwa zikipigiwa kelele na wananchi.

Moja ya mambo yanayolalamikiwa kwenye sheria hiyo ni kuwepo kwa vipengele vinavyobana waandishi wa habari, ambapo mwandishi akitaka kupata taarifa yeyote toka kwenye mamlaka za kiserikali, anaweza kukaa ndani ya siku 30 bila kutoa habari, ambapo kwa mazingira kama hayo ni wazi kuwa hakutakuwa na habari tena kwa wananchi.

Katibu mkuu wa chama hicho Abdulrahman Kinana, ameendelea kusisitiza kuwa sheria nyingi nchini zimekuwa zikitungwa bila kuwashirikisha wananchi ambao wameiweka serikali madarakani na serikali ipo kwaajili ya wananchi na si wananchi kwaajili ya serikali.

Akiwa katika wilaya ya Misungwi mkoani Mwanza, katika mwendelezo wa ziara ya chama hicho ya kukagua utekelezaji wa ilani ya uchaguzi ya mwaka 2010, katibu mkuu huyo aliuagiza uongozi wa wilaya ya misungwi, kugawa chakula cha msaada toka serikalini bila upendeleo ambapo wilaya hiyo inakabiliwa na njaa kufuatia mvua zilizonyesha hivi karibu kuharibu sehemu kubwa ya mazao ya
wananchi.

No comments: