MFANYABIASHARA maarufu Marijan Abubakar ‘Papa Msofe’ na mwenzake, Makongoro Joseph, wamefutiwa kesi ya mauaji iliyokuwa inawakabili katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu.
Hata hivyo, baada ya kuachiwa, Msofe alikamatwa tena na kufunguliwa kesi nyingine ya kughushi na kuwasilisha nyaraka za uongo.
Hakimu Mkazi, Renatus Rutta aliwaachia huru washitakiwa hao baada ya
kufuta kesi hiyo chini ya kifungu cha 91 (1) cha Sheria ya Mwenendo wa
Makosa ya Jinai (CPA).
Kesi hiyo imefutwa kwa kuwa Mkurugenzi wa Mashitaka nchini (DPP)
aliwasilisha hati ya kutokuwa na nia ya kuendelea kuwashitaki
washitakiwa hao. Msofe na Makongoro wamesota rumande kwa zaidi ya miaka
miwili kwa kuwa upande wa Jamhuri ulikuwa unadai upelelezi wa kesi
haujakamilika.
Msofe kwa mara ya kwanza alifikishwa mahakamani, Agosti 2012 na
Makongoro Februari 2013. Baada ya kuachiwa Makongoro aliruhusiwa
kuondoka katika eneo la mahakama na Msofe alipandishwa kizimbani mbele
ya Hakimu Rutha na kusomewa mashitaka mawili.
Katika mashitaka hayo, Msofe anadaiwa Desemba 23, 2004 katika Wilaya
ya Ilala kwa nia ya kudanganya alighushi nyaraka ya kuhamisha haki ya
umiliki wa nyumba namba 288 ambayo ni mali ya aliyekuwa mfanyabiashara
wa madini, Onesphory Kituli (sasa marehemu).
Ilidaiwa kuwa Msofe kwa nia ya kudanganya alighushi nyaraka hiyo
akionesha Desemba 13, 2004 Kituli alihamisha haki yake ya umiliki wa
nyumba hiyo kwake wakati akijua ni uongo.
Katika mashitaka mengine, inadaiwa kati ya Desemba 23, 2004 na Machi
30, 2005 kwa nia ya kudanganya, Msofe alitoa nyaraka hizo za uongo kwa
Kamishna wa Ardhi kwa lengo la kuhamisha umiliki kutoka kwa Kituli
kwenda kwake.
Upelelezi wa kesi hiyo haujakamilika na dhamana kwa mshitakiwa ipo
wazi endapo atatimiza masharti ya kuwa na wadhamini wawili wa kuaminika
watakaosaini hati ya Sh milioni 10 kila mmoja. Kesi itatajwa tena Julai
9, mwaka huu.
No comments:
Post a Comment