Mpekuzi blog
KESI ya wizi wa silaha aina ya SMG na risasi zake 42 inayomkabili
aliyekuwa Konstebo wa Polisi, GX 7274, Hamad Taimu Shilingi (25) katika
Mahakama ya Wilaya ya Sumbawanga mkoani Rukwa imeahirishwa hadi Julai
Mosi mwaka huu.
Hakimu wa Mahakama hiyo, Enock Matembele aliamuru mshtakiwa arudishwe
rumande hadi Julai Mosi mwaka huu ambapo mahakama hiyo itaamua iwapo
mshtakiwa huyo apewe dhamana au la.
Mshtakiwa huyo alifikishwa mara ya kwanza Mei 26 mwaka huu ambapo
upande wa mashtaka ulipinga asipatiwe dhamana kwa kuwa bado upelelezi wa
shauri hilo unaendelea ambapo upande wa utetezi uliwasilisha mahakamani
hapo kiapo cha pingamizi .
“Uamuzi kuhusu mshtakiwa apewe dhamana au la utatolewa na Mahakama
hii hapo Julai Mosi mwaka huu hivyo mshtakiwa atarudi rumande hadi
tarehe hiyo,“ alieleza Hakimu Matembele mahakamani hapo.
Kwa mujibu wa hati za mashtaka mahakamani hapo mshtakiwa alitenda
kosa hilo Aprili 4 , mwaka huu katika Kituo cha Polisi mjini Namanyere
wilayani Nkasi ambapo anadaiwa kuiba silaha aina ya SMG yenye nambari
21084.
Ilidaiwa mahakamani hapo kati ya Aprili 04 na Mei 19 mwaka huu
mshtakiwa huyo aliiba risasi 42 za SMG kutoka katika kituo kikuu hicho
cha Polisi mjini Namanyere wilayani Nkasi.
Kabla ya kufikishwa mahakamani hapo kwa mara ya kwanza, Mei 26 mwaka
huu mbele ya Hakimu Matembele, mshtakiwa huyo Mei 22 alifikishwa na
kuhukumiwa katika Mahakama ya Kijeshi.
No comments:
Post a Comment