OFISI ya
Taifa ya Takwimu imetoa makadirio ya idadi ya watu wanaotarajiwa kupiga
kura katika uchaguzi mkuu wa Oktoba 2015 ambao wanakisiwa kuwa watafikia
milioni 24.2 nchi nzima.
Taarifa
hizo ni makadirio ya idadi ya watu wanaostahili kupiga kura katika
majimbo ya uchaguzi Tanzania kwa mwaka 2015. Katika uchaguzi mkuu wa
mwaka 2010, idadi ya wapigakura waliojiandikisha ilikuwa 20,137,303,
lakini waliopiga kura Oktoba 31 mwaka huo walikuwa 8,626,283 sawa na
asilimia 42.84 ya wapiga kura wote waliojiandikisha.
Takwimu
hizi zimetolewa katika ngazi ya Mkoa, Wilaya, Jimbo la Uchaguzi na Kata
au Shehia kama yalivyokuwa mwaka 2010. Makadirio ya idadi ya wapigakura
yametokana na Sensa ya Watu na Makazi ya Mwaka 2012.
Kwa
mujibu wa ripoti iliyo kwenye kitabu maalumu cha takwimu za wapiga kura
mwaka huu, ambayo nakala yake imepatikana kupitia Ofisi ya Takwimu ya
Mkoa wa Arusha, idadi hiyo imepatikana kwa kutumia mbinu za kidemografia
zinazohusisha mabadiliko katika viwango vya uzazi, vifo, uhamaji na
uhamiaji katika ngazi ya Taifa, Mkoa, Wilaya, Majimbo ya Uchaguzi na
Kata au Shehia husika.
Inakadiriwa
kuwa ifikapo siku ya uchaguzi, Tanzania itakuwa na watu wapatao
48,522,229 ambapo watakaokuwa na umri wa kupiga kura watakuwa ni watu
24,252,927 iwapo wote watafanikiwa kuandikishwa upya.
Mkoa wa
Dar es Salaam wenye majimbo nane unatarajiwa kuwa na wapiga kura wengi
zaidi watakaofikia milioni 3, ukifuatiwa na Mbeya itakayokuwa na wapiga
kura milioni 1.5, Mwanza milioni 1.4 na Morogoro itakayokuwa na
wapigakura milioni 1.3 katika nafasi ya nne.
Mikoa
mingine inayotarajiwa kuwa na wapiga kura wengi ni pamoja na Kagera
itakayokuwa na wapigakura milioni 1.2, Tabora inayokadiriwa kuwa na
idadi ya wapiga kura milioni 1.1, Tanga nayo kwa idadi kama hiyo ya
milioni 1.1 pamoja na Dodoma itakayokuwa na wastani wa wapigakura
milioni moja.
Mkoa wa
Kilimanjaro unatarajiwa kuwa na wapiga kura 976,000 katika nafasi ya
tisa na hatimaye Arusha kufunga kumi- bora ikiwa na matarajio ya wapiga
kura wapatao 944,000. Idadi ya wapigakura watarajiwa kwa mikoa mingine
ni kama ifuatavyo:
Mara
(834,000), Geita (808,000), Ruvuma (783,000), Mtwara (773,000),
Shinyanga (762,000), Manyara (741,000), Simiyu (714,000), Singida,
(698,000), Pwani (644,000), Iringa (524,000), Rukwa (472,000) na Njombe
(393,000).
Mkoa mpya
wa Katavi, ambao una idadi ya wakazi wapatao 609,000 ndio utakuwa na
idadi ndogo zaidi ya wapigakura kwa Tanzania bara wakitarajiwa kuwa
271,000. Huko visiwani mkoa wa Mjini Magharibi unatarajiwa kuwa na
wapigakura 347,000, Kaskazini Unguja 104,000, Kaskazini Pemba 103,000,
Kusini Pemba 95,000 na Kusini Unguja 69,000.
Maandalizi
ya kitabu cha idadi tarajiwa ya wapigakura yameshirikisha maofisa
kutoka Wizara, Idara na Taasisi za Serikali ikiwemo Ofisi ya Taifa ya
Takwimu na Ofisi ya Mtakwimu Mkuu wa Serikali Zanzibar, pamoja na Ofisi
ya Waziri Mkuu - Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Tume
ya Taifa ya Uchaguzi, Tume ya Uchaguzi Zanzibar na Chuo cha Takwimu
Mashariki mwa Afrika (EASTC).(HABARI LEO)
No comments:
Post a Comment