Wanachama
wa chama cha Wamiliki wa Vyombo vya Habari nchini – MOAT na wadau
wengine wa habari wameazimia kuishauri serikali kuondoa bungeni muswada
wa sheria ya upatikanaji wa habari ili kulinda na kudumisha amani,
utulivu na demokrasia.
Maazimio hayo yamefikiwa jijini Dar es salaam wakati wa mkutano wa
Wanachama wa MOAT na wadau wengine wa habari, baada ya kupata ufafanuzi
wa kina kuhusu muswada wa sheria hiyo kutoka kwa mwanasheria mwandamizi
Dr Damas Ndumbaro, na baadaye wajumbe kuujadili na wazohatimaye
kuafiki wazo lililotolewa na Mmiliki wa New Habari Corporation Bw.
Rostam Aziz.
Mapema Mwenyekiti wa MOAT Dr Reginald Mengi alitahadharisha kuwa
hakuna mtu binafsi atakayeweza kuendesha vyombo vya habari iwapo muswada
huo utapitishwa kuwa sheria bila ya kufanyiwa marekebisho.
Aidha Dr Mengi pia ameshangazwa na udharura wa kutungwa kwa sheria
hiyo wakati huu wa kuelekea uchaguzi mkuu, na kusisitiza kuwa amani na
utulivu unaweza kupotea na uchaguzi hauwezi kuwa huru iwapo vyombo vya
habari vinanyimwa uhuru wa kupata habari na kuutangazia umma.
Akichanganua kuhusu utata wa muswada huo Mwanasheria Dr Damas
Ndumbaro na Mwandishi wa Habari wa the Citizen wamesema muswada huo
pamoja na mambo mengine, unamtaka mwandishi wa habari anayetafuta habari
kupeleka maombi rasmi yatakayojibiwa katika kipindi cha siku 30, na
inapoteza ajira kwa waandishi wa habari.
No comments:
Post a Comment