Serikali ya Somalia imetangaza kuwa watu waliouawa katika mapigano yaliyoibuka katika mpaka wa nchi hiyo na Ethiopia imeongezeka na kufikia 50.
Taarifa iliyotolewa na viongozi wa serikali ya Somalia imeeleza kuwa wahanga hao wanatoka pande mbili baina ya wanamgambo wa Ethiopia na wale wa Somalia.
Hii ni katika hali ambayo awali viongozi na wakuu wa makabila nchini Somalia walikuwa wametangaza kuuawa watu wasiopungua 35 ambao ni raia kwenye mapigano ya wiki iliyopita katika vijiji vya maeneo ya kando na mpaka wa Somalia na Ethiopia.
Hussein Weheliye Irfo, kamanda wa eneo la Galgadud, la katikati mwa Somalia amesema kuwa, wengi wa wahanga wa mapigano hayo ni raia wa kawaida. Kwa mujibu wa Hussein, mapigano hayo yaliibuka baada ya mtu mmoja kutoka kundi la jeshi la polisi la Ethiopia maarufu kwa jina la LIYU kushambulia mkusanyiko wa mabedui wa Somalia, suala lililopelekea kuibua mapigano makali na kuuawa watu 50 wakiwamo wanawake 11.
Inaelezwa kuwa, mamia ya wanavijiji wamelazimika kukimbilia maeneo mengine yenye amani kukhofia usalama wao. Kwa mujibu wa baadhi ya duru za habari, mapigano hayo yaliibuka siku ya Ijumaa na kuendelea hadi Jumamosi iliyopita.
No comments:
Post a Comment