Halfa ya kuapishwa kwa makatibu wakuu na naibu makatibu wakuu 26 iliyofanyika jana Ikulu Jijini Dar es Salaam ilikuwa ya aina yake kutokana na kuapa mara mbili, huku Rais John Magufuli akiwaeleza kuwa asiyeweza kazi aseme asile kiapo, akae kando.
“Inawezekana tulizungumza kwa ujumla lakini kumbe si wote wanakubali masharti kuhusu rushwa, kutoa vitu vya upendeleo. Kwa hiyo, niwaombe makatibu wakuu pamoja na kwamba mlishaapa kwangu, ambaye hakubaliani na hilo asimame kando ili waliobaki waendelee,” alisema Rais Magufuli kabla ya kiapo cha pili cha uadilifu.
Hakuna aliyesema hawezi kazi hivyo wote walikula kiapo hicho.
Baada ya hapo, Balozi Sefue aliwataka kunyanyua mikono yao juu na kusoma kiapo hicho cha uadilifu kwa sauti: “Mnakula kiapo hiki kulingana na makubaliano, kwamba ukiwa mtumishi wa Serikali lazima ukubali kusaini fomu hii inayoashiria kuwa kiongozi ana dhamana kubwa kwa nchi na wananchi.”
Katika kiapo hicho cha pili, walisaini hati ya ahadi ya uadilifu kwa viongozi wa umma, inayotolewa na Ofisi ya Rais, Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma.
Sehemu ya kiapo hicho,chenye vipengele 12 inasema; "Nitakuwa mzalendo kwa nchi yangu na mtii kwa serikali ya Jamhuri Ya Muungano wa Tanzania;Sitatumia Cheo changu au Wadhifa wangu kwa maslahi binafsi ya familia yangu,ndugu zangu au marafiki zangu isipokuwa kwa maslahi ya umma"
Kiapo hiki cha pili cha maadili ya viongozi wa umma kiliwahusisha pia makatibu na naibu makatibu wakuu 24 wa zamani, hivyo kufanya jumla yao kuwa 50 wa wizara mbalimbali walioteuliwa na Rais Magufuli Desemba 30 mwaka jana.
Makatibu wakuu waliohusika kuapa kiapo cha kwanza walikuwa 12 na naibu makatibu wakuu 14 wote wakiwa wale walioteuliwa kwa mara ya kwanza. Makatibu wakuu na naibu makatibu wakuu 24 ni wale waliohamishwa na walioendelea na wizara zao.

No comments:
Post a Comment