Kocha mkuu wa zamani wa Free State ya Afrika Kusini, Kinnah Phiri amekubari kujiunga na kikosi cha Mbeya City Fc kwa mkataba wa miaka mitatu, kuanzia leo hii.
Kwenye mazungumzo ya siku mbili yaliyofanyika kwenye ofisi za klabu zilizopo jengo la Mkapa Hall jijini hapa, Kocha Phiri amesaini kandarasi hiyo ya kuwa kocha mkuu kwa kipindi hicho na kuahidi ujenzi mpya wa kikosi mara baada ya kumalizika kwa msimu huu wa 2015/16.
“Nashukuru, nimekuwa hapa kwa siku mbili, mazungumzo yamekamilika jioni hii, sasa nitaongoza kikosi hiki kwa miaka mitatu ijayo, limekuwa ni jambo zuri kwangu kufanya kazi Tanzania kwa mara ya kwanza, City ni moja ya timu nzuri zenye hamasa kubwa kwenye soka la nchi hii, jitihada zangu za mwanzo zitakuwa ni kuhakikisha inasalia kwenye ligi ili tujenge kikosi kipya cha mafanikio msimu ujao” alisema Kocha Phiri.
Aidha kocha huyo aliyewahi kuifundisha kwa mafanikio timu ya taifa ya Malawi (The Flames) amefurahishwa na uwepo wa nyota waliotamba kwenye soka la Tanzania kwa muda sasa akiamini watakuwa sehemu ya mafaniko ya kazi yake kwenye kikosi cha City.
“Siku chache kabla sijafika hapa nilipata habari za kuwepo kwa Juma Kaseja na Haruna Moshi kwenye timu hii, hawa ni wachezaji ambao mwalimu yeyote angependa kufanya nao kazi, nafahamu juu ya uwezo na vipaji vyao naamini watakuwa sehemu ya mafanikio kwangu na kikosi kizima, leo hii nimepata nafasi ya kuona mazoezi timu ina wachezaji wengi vijana, wana vipaji vya hali ya juu, sina shaka timu hii itakuwa moja ya timu za kuogopwa” alisema.
Kwa upande wake katibu mkuu wa City Emmanuel Kimbe amesema kuwa amefurahishwa na makubaliano yaliyofikiwa na kocha huyo raia wa Malawi huku akiahidi kumpa ushirikiano mkubwa katika kuhakikisha timu inarudia makali yake ya awali.
“Nimefurahi, makubaliano mazuri yamefikiwa, timu yetu sasa ina mwalimu wa kiwango cha juu kabisa , kwetu sisi uongozi tunaahidi kumpa ushirikiano mkubwa ili kufanikisha malengo ya pande zote”.
Kuhusu kocha aliyekuwepo kabla Kimbe amesema kuwa kwa sasa bado hawezi kutoa tamko lolote kuhusu aliyekuwa kocha mkuu meja mstaafu Abdul Mingange mpaka hapo baadae.
“Siwezi kusema lolote kwa sasa kuhusu kocha aliyekuwepo, nadhani ni vyema tusubiri kwa sababu kuna kikao cha bodi juma lijalo baada ya hapo taarifa itatolewa” alimaliza
No comments:
Post a Comment