Friday, 10 June 2016

UKAWA Wamjibu Naibu Spika.....Wamwambia Posho akawatishie watoto


Siku mbili baada ya Naibu Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. Tulia Ackson kuagiza wabunge wa upinzani wanaoingia Bungeni na kisha kuondoka wakisusa vikao wasilipwe posho, wabunge hao wamejibu wakiubeza na kuupinga uamuzi huo.

Wakiongea kwa nyakati tofauti, wabunge wa upinzani wamekosoa uamuzi huo wakieleza kuwa Dk. Tulia alihukumu kesi inayomhusu, kitendo walichosema sio haki.

Aidha, wabunge hao walieleza kuwa posho haitakuwa sababu ya kuwarudisha nyuma kwenye uamuzi wao kwakuwa sio hoja wanayoipigania. Walisisitiza kuwa wataendelea kutoshiriki vikao vya Bunge vinavyoongozwa na Dk. Tulia kama walivyoazimia.

“Ukawa haiwezi kutishiwa posho tunapokuwa na hoja na mawazo ya msingi. Hoja yetu hapa si posho, kuna mambo ambayo anayafanya Naibu Spika hayaendi sawa na sio ya kawaida. Hoja ya posho akawatishie watoto, sisi ni watu wazima. Tumekuja hapa tuna utashi mkubwa,” alisema Mbunge wa Ukonga, Mwita Waitara (Chadema).

Naye Mbunge wa Vunjo na Mwenyekiti wa NCCR-Mageuzi, James Mbatia alisema kuwa uamuzi wa Naibu Spika unawadhalilisha wabunge kwa kuonesha kuwa posho ndio kitu walichokifuata Bungeni hapo.

“Mimi nimekuwa kwenye siasa kwa miaka zaidi ya 25 sasa. Kilichofanywa na Naibu Spika ni kudhalilisha wabunge, ionekane sasa tupo hapa kwa ajili ya kulipwa posho. Tupo hapa kwa ajili ya kutoa huduma kwa Watanzania. Kina Tulia wakiwa shule ya msingi, sisi tunapambana bila kulipwa posho na mtu yoyote,” alisema Mbatia.

Kiongozi wa Kambi rasmi ya upinzani Bungeni, Freeman Mbowe alitoa msimamo wa kambi hiyo kuwa hawatashiriki vikao vyote vya Bunge vinavyoongozwa na Naibu Spika kwakuwa amekuwa wakiwakandamiza na kupendelea upande mmoja. Pia, Mbowe alisema kuwa Dk. Tulia anaongoza Bunge kwa ubabe akilinda maslahi ya Serikali.

No comments: