Thursday, 24 August 2017

Adakwa kisa noti bandia za laki sita


JESHI la Polisi Mkoa wa Kigoma linamshikilia Paul Shishi (47), mkazi wa Nyabusuzi Wilaya ya Biharamulo mkoani Kagera, kwa tuhuma za kukutwa na noti bandia 63 za Sh. 10,000 zenye thamani ya fedha halali (Sh. 630,000).

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kigoma, Ferdinand Mtui, alisema tukio hilo lilitokea juzi mchana katika Kijiji cha Kibingo Kata ya Kaziguzigu Wilaya ya Kakonko mkoani hapo.

Mtui alisema askari polisi wakiwa doria walipokea taarifa kutoka kwa raia wema wanaochukia uhalifu na wahalifu kwamba kuna mtu mmoja ana fedha nyingi ambazo wanazitilia shaka kama ni halali.

Alisema baada ya askari hao kupokea taarifa hizo walikwenda katika eneo la tukio na kumkamata Shishi akiwa na noti bandia 63 za Sh. 10,000 zenye thamani ya fedha halali Sh. 630,000 kitendo ambacho ni kinyume cha sheria.

Kamanda Mtui alisema upelelezi wa kesi hiyo umekamilika na jalada limepelekwa kwa mwanasheria na likitoka huko mtuhumiwa huyo atafikishwa mahakamani, ili sheria iweze kuchukua mkondo wake.

Aidha Kamanda Mtui aliwataka wananchi kuendelea kutoa taarifa katika vituo vya polisi za uhalifu na wahalifu mara moja pindi wanapokuwa na shaka dhidi ya mtu au kundi la watu, ili hatua za kisheria ziweze kuchukuliwa mara moja kabla uhalifu haujafanyika.

No comments: