Thursday, 17 August 2017

Akamatwa na Polisi kwa kumpaka mwanae kinyesi


SeeBait
Mtu mmoja anashikiliwa na Jeshi la Polisi kwa kosa la kumfanyia ukatili mtoto wake wa kumpaka mavi ya mbuzi kwenye majeraha aliyoungua na  moto wilayani Nyamagana.

Kwamba tarehe 15.08.2017 majira ya saa 16:30hrs jioni katika Mtaa wa Chakechake – Mkuyuni Wilaya ya Nyamagana Jiji na Mkoa wa Mwanza, Sospeter Rajabu miaka 42, mvuvi na mkazi wa mtaa wa Chakechake – Mkuyuni, anashikiliwa na jeshi la polisi kwa kosa la kumfanyia ukatili mtoto wake aitwaye Neema Sospeter miaka 10, mwanafunzi wa darasa la kwanza, wa kumpaka mavi ya mbuzi kwenye majeraha ya moto aliyoungua maeneo ya mapaja ya miguu yote miwili kwa muda wa wiki mbili na kupelekea majeruhi kuwa na hali mbaya kiafya, kitendo ambacho ni kinyume na sheria.

Inadaiwa kuwa tukio hilo la ajali ya moto dhidi ya mtoto lilitokea tarehe 04.08.2017 majira ya saa 19:45hrs usiku, katika mtaa wa Kitangiri wilayani Ilemela ambapo majeruhi alikuwa akiishi na mama yake kwani wazazi wake walitengana kwa muda mr

Inasemekana ajali hiyo ya moto ilitokea baada ya majeruhi kumwagikiwa na mafuta ya taa pindi alipokuwa akiweka kwenye taa ya kibatari ndipo alipowasha moto na njiti ya kibiriti moto ulilipuka na kumuunguza kwenye maeneo hayo.

Inasemekana kuwa baada ya mama wa mwenye mtoto kukosa fedha za matibabu aliamua kumpeleka mtoto kwa baba yake Mtaa wa Chakechake – Mkuyuni alipokua akiishi na mke mwingine ili amsaidie mtoto apate matibabu, lakini inadaiwa kuwa baada ya mtoto kufikishwa kwa baba yake hakupelekwa hospitali badala yake alikuwa akipakwa mavi ya mbuzi na kupelekea hali yake kuzidi kuwa mbaya.

Wananchi walitoa taarifa polisi kuhusiana na tukio hilo, ambapo askari walifanya ufuatiliaji wa haraka hadi maeneo hayo na kufanikiwa kumkuta mtoto  akiwa kwenye hali ngumu.  Askari kwa kushirikiana na wananchi walimchukua mtoto huyo na kumkimbiza Hospitali ya Mkoa ya Sekou Toure kupatiwa matibabu huku baba wa mtoto Sospeter Rajabu akitiwa nguvuni.

Polisi wapo kwenye upelelezi na mahojiano na mtuhumiwa dhidi ya ukatili aliyokuwa akimtendea mwanae, pindi uchunguzi ukikamilika mtuhumiwa atafikishwa mahakamani.

Majeruhi amelazwa Hospitali ya Mkoa ya Sekou Toure akiendelea kupatiwa matibabu na hali yake inaendelea vizuri.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza Naibu Kamishina wa Polisi Ahmed Msangi anatoa wito kwa wananchi wa Mkoa wa Mwanza, kuwa pale ambapo kunatokea mtoto au mtu yeyote anapata majeraha au kuungua ni vizuri wakawaone madaktari katika hospitali ambapo wanaweza kupata huduma bora na stahiki za matibabu kuliko kutumia njia za kienyeji zisizofaa ambazo hazina ubora/usahihi, kwani kufuata njia ambazo si sahihi na bora kunaweza kupelekea kifo kwa mgonjwa.

Imetolewa na;

DCP: Ahmed Msangi

Kamanda wa Polisi (M) Mwanza

No comments: