Zaidi
ya wanafunzi 30,000 wa vyuo vya elimu ya juu nchini kwa mwaka mpya wa
masomo 2017/18, watanufaika na Sh bilioni 427 kutoka Bodi Mikopo ya
Elimu ya Juu (HESLB), huku wanufaika hao wakiwekwa kwenye mikondo
mitatu.
Jana
Mkurugenzi Mtendaji wa HESLB, Abdul –Razaq Badru alisema kwa mwaka huu
wanufaika wasiopungua 30,000 watapata mikopo ya elimu kulingana na fani
walizochagua kusoma.
Akifafanua
idadi na kiwango cha mkopo kitakachotolewa kwa kila mkondo kulingana na
fani watakazosoma, Badru alisema bodi imepanga mikondo mitatu ya
mikopo.
Mkondo
wa kwanza unawahusu wanafunzi wa fani za afya, sayansi ya elimu na
hesabu, ambapo kundi hilo litapata asilimia 40 ya mkopo huo ambao ni
sawa na Sh bilioni 170.8.
Badru
alisema kundi hilo ndilo litapata mkopo mkubwa kuliko makundi mengine
kutokana na fani hizo kuwa adimu na zina mahitaji makubwa ya soko nchini
hasa kwa kuwapata wataalamu watakaosaidia taifa kwenye sekta za afya,
sayansi na elimu.
Mkondo
wa pili umepangwa kupata asilimia 35 ya mkopo wote ambao ni sawa na Sh
bilioni 149.45 na wanafunzi watakaonufaika ni wale wa fani za uhandisi,
kilimo, misitu, sayansi ya ardhi, usafirishaji na fani kama hizo.
Mkondo
wa tatu umepangwa kupata asilimia 25 ya mkopo wote ambao ni sawa na Sh
blioni 106.75 na wanufaika wa mkopo huo ni wanafunzi wote watakaosoma
fani za lugha, sanaa, jamii na fani nyingine kama hizo.
Badru
alisema pamoja na bodi kuweka mikondo hiyo, lakini pia suala la jinsia
litazingatiwa ili kuepusha jinsi moja kuwa na idadi kubwa ya wanufaika
wa mikopo hiyo.
Katika
hatua nyingine kwa mwezi mmoja uliopita, bodi hiyo imekusanya marejesho
ya mkopo ya Sh bilioni 31.1 huku ikiweka mikakati ya mwaka huu ya
kukusanya kila mwezi zaidi ya Sh bilioni 14.
Mtendaji
huyo wa HELSB alisema lengo lao ni kuhakikisha wanufaika wote
wanafikiwa na kurejesha madeni yao ili yasaidie wengine kupata elimu.
Alisema
mikakati yaliyojiwekea kuanzia mwaka huu ni kukusanya zaidi ya Sh
bilioni 14 kila mwezi na kwamba tangu mwaka huu wa fedha uanze, kwa
mwezi Julai pekee wamekusanya Sh bilioni 31.1 huku sekta ya umma
ikiongoza kwa wanufaika wake kurejesha madeni yao.
“Tunakwenda
vizuri na tumejiwekea mikakati ya kuhakikisha madeni ya mikopo hiyo
yanarejeshwa ili yaweze kunufaisha wengine, kwa sekta ya umma
tumefanikiwa kuwafikia asilimia 82 ya wadaiwa wote na sekta binafsi
tumefanikiwa kwa asilimia arobaini,” alisema Badru.
Aliongeza
kuwa hivi sasa wameweka nguvu kwenye sekta binafsi, kwa kuwa imekuwa
vigumu kuwafikia wadaiwa wote kutokana na sekta hiyo waajiriwa wake
kuhamahama kila wakati au kuacha kazi.
Akizungumzia
mikakati ya kukusanya madeni ya mikopo hiyo, Badru alisema wapo mbioni
kuanzisha kampeni ya ‘’Kurejesha mkopo ni uzalendo uliotukuka’’,
itakayofanywa nchi nzima kuhamasisha wanufaika wa bodi hiyo kujenga
tabia ya kurejesha kwa hiari madeni yao.
Alitaja
mkakati mwingine ni bodi hiyo hivi sasa iko kwenye hatua za awali za
mazungumzo na taasisi za fedha nchini ili kuona jinsi ya wao kununua
mikopo hiyo ya wadaiwa kupitia waajiri wao.
Awali
operesheni ya utafutaji, ufuatiliaji na ukaguzi wa wadaiwa sugu wa bodi
hiyo mahala pa kazi yaliyoendesha mapema mwaka huu kwa kipindi cha
mwaka mmoja uliopita, ilifanikiwa kwa kukusanya Sh bilioni 116 ikiwa ni
kiwango cha marejesho cha asilimia 46, huku awali walilenga kukusanya Sh
bilioni 76.
Hata
hivyo, aliwakumbusha waajiri wote nchini kuhakikisha wanatoa taarifa za
waajiri wanaodaiwa na bodi hiyo na kuhakikisha wanakata asilimia 15 ya
mshahara yao na kuipeleka bodi ili kulipa madeni yao
Credit:Habari leo
No comments:
Post a Comment