Jeshi
la Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam limeanza kutekeleza operesheni
iliyoitangaza wiki iliyopita kwa kuwaondoa wapigadebe kwenye vituo vya
daladala kutokana na kuwa chanzo cha wizi.
Kaimu
Kamanda wa Kanda Maalum Dar es Salaam, Lucas Mkondya, jana alisema
kuwa, operesheni hiyo imeanza jijini baada ya kukithiri kwa kesi
zitokanazo na wizi kwenye vituo hivyo.
Alisema
kwa siku kunaripotiwa matukio 20 hadi 50 ya wizi kwenye vituo vya
daladala jijini huku wapigadebe wakidaiwa kuwa kichaka cha wizi huo.
Alisema operesheni hiyo, itakayoendeshwa kwa wiki nzima imelenga kuvifanya vituo hivyo kuwa maeneo salama.
“Vituoni
kunakuwa na wizi na wezi wanafahamika, sasa ni mkakati wa kuwaondoa na
kama wiki ikimalizika wizi haujaisha, tutawaondoa wote ambao hawana
shughuli maalum vituoni hata kama hawapigi debe,” alisema.
Agizo
la Kamanda Mkondya si jipya hata hivyo kwa wapiga debe baada ya
maazimio kama hayo, kadhaa kushindwa katika miaka ya nyuma.
Akizungumza
Machi 16, mwaka jana jijini, Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za
Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), George Simbachawane alimtaka Mkuu
wa Mkoa wa Dar es Salaam kuhakikisha anawaondoa wapiga debe wote kwenye
vituo vya mabasi kwa sababu hizo hizo.
Waziri
Simbachawene alitoa agizo hilo, wakati wa semina kwa wakuu wa mikoa
wote nchini ambao walikuwa wameapishwa na Rais John Magufuli, Ikulu
katika siku iliyotangulia.
Waziri
huyo, alisema kazi ya kupiga debe sio rasmi na isiyo na kipato
kitachoweza kumkwamua kijana husika kuondokana na umaskini.
“Namuomba
Mkuu wa Mkoa ahakikishe anawaondoa hawa wapiga debe kwenye vituo vya
mabasi kwa kuwa wamekuwa wakichangia kutokea kwa uhalifu," alisema Simbachawene.
"Kipato cha mpiga debe kwa siku hakiwezi kumkwamua kimaisha, sana sana wanatumia nafasi hiyo, kufanya uhalifu.
Wanatakiwa kuondolewa haraka waende kwenye kazi hata za kilimo.”
No comments:
Post a Comment