Bukombe. Ofisa Mtendaji wa Kijiji cha Ihulike
wilayani Bukombe, Lucas Maganga amefikishwa katika mahakama ya wilaya
kwa tuhuma ya rushwa.
Akimsomea shtaka hilo mwishoni
mwa wiki iliyopita mbele ya Hakimu Mfawidhi wa mahakama hiyo, Gabriel
Kurwijila, Mwendesha Mashtaka wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na
Rushwa (Takukuru) wa wilaya hiyo, Kelvin Murusuri alidai Maganga
alitenda kosa hilo Julai kwa tarehe na nyakati tofauti.
Alidai
kuwa baada ya mshtakiwa kupata taarifa za ujauzito wa mwanafunzi wa
darasa la saba katika Shule ya Msingi Ihulike, alizikutanisha familia
mbili za upande wa msichana na mvulana aliyempa ujauzito kisha
akizishawishi zielewane.
Aliendelea kuiambia mahakama
kuwa baada ya ushawishi huo, Stephano Maliyatabu ambaye ni mzazi wa
mvulana alitoa Sh950,000, kati ya fedha hizo mtendaji alipewa Sh450,000
na nyingine alipewa mzazi wa msichana huyo. Hata hivyo, mshtakiwa
alikana shtaka hilo na upande wa mashtaka ulidai uchunguzi umekamilika.
Mshtakiwa alikosa wadhamini wawili waliopaswa kusaini dhamana ya Sh3
milioni kila mmoja na hivyo kukosa dhamana. Kesi hiyo iliahirishwa hadi
Oktoba 12.
Credit ; Mwananchi.
Credit ; Mwananchi.
No comments:
Post a Comment