WANANCHI WA WILAYA YA ILEJE,KUSIMAMIA MIRADI YA SEKTA YA AFYA NA KUFUATILIA MATUMIZI SAHIHI YA FEDHA ZA UMMA.
Na Ester Macha,Ileje.
Serikali
wilayani Ileje Mkoani Mbeya imesema kuwa baada ya kuwepo kwa malalamiko
ya kutokamilika kwa miradi ya sekta ya afya inayoelekezwa na fedha
zinazotolewa na Serikali sasa miradi hiyo kusimamiwa na wananchi wenyewe
na kufuatilia matumizi sahihi ya fedha za umma.
Kauli hiyo ilitolewa wiki
iliyopita na Mkuu wa Wilaya ya Ileje Bi.Rosemary Senyamule wakati
akizindua mradi utakaowashirikisha wananchi na kuwajengea uwezo ili
waweze kuwajibika katika miradi yao katika maeneo yao na kufuatilia
matumizi sahihi ya fedha zinazotolewa kwa ajili ya miradi hiyo.
Alisema kuwa mradi huo
unadhadhiliwa na(FOUNDATION FOR CIVIL SOCIETY)ambao utaweza kusaidia
miradi mingi ya sekta ya afya ambayo imekuwa ikilalamikiwa na wananchi
kutokana na kutokamilika kwa wakati na matumizi yake kutokuwa sahihi na
hivyo wananchi kuzua maswali mengi.
Akizungumza wakati wa uzinduzi
huo Mkurugenzi wa Shirika la Hossan Ows Center Bw.Nsanya Mwalyego
alisema kuwa katika ripoti ya utekelezaji wa miradi ya maendeleo ya
sekta ya afya wilayani Ileje iliyotolewa na Idara ya afya kwa mwaka
2010/2011 inaonesha miradi mingi wilayani humo imeshindwa kukamilika
licha ya serikali kuu kuelekeza fedha katika miradi hiyo.
Alisema kuwa baadhi ya wananchi
ambao ndio walengwa wa kuletewa miradi na serikali wameonesha kutokuwa
wawajibikaji katika miradi yao na hivyo kusababisha kuwa hafifu licha ya
kuwa wanatakiwa kuwajibika katika miradi yao ya maendeleo ambayo
imeletwa kwa ajili ya kusaidia wananchi.
Mmoja wa wananchi wa Wilaya ya
Ileje Bw. Kasele Msongole alisema kuwa kuanzia sasa watakuwa mstari wa
mbele katika kusimamia miradi ya afya ambayo inatolewa na serikali,mara
nyingi fedha za miradi zimekuwa zikishindwa kufanya kama ilivyolengwa
kutokana na walengwa wenyewe kutokuwa makini na miradi yao.
Hata hivyo Mkuu wa Wilaya hiyo
amewapa jukumu wananchi la kuimarisha mradi wa kuimarisha uwajibikaji wa
jamii ya Ileje katika kusimamia mipango ya maendeleo ya sekta ya afya.
No comments:
Post a Comment