Wednesday, 24 June 2015

Mfanyabiashara Wa Madini Apigwa Risasi Arusha


MFANYABIASHARA maarufu wa madini ya tanzanite jijini Arusha, Mathias Manga amepigwa risasi nyumbani kwake juzi usiku na watu wasiojulikana. Polisi imethibitisha tukio na kwamba majeruhi anaendelea vizuri na matibabu.
 
Akizungumza na waandishi  wa  habari, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha Liberatus Sabas alikiri kutokea kwa tukio hilo na kusema kuwa Manga amepigwa risasi ubavuni saa 4.45 usiku nyumbani kwake Ngarenaro alipokuwa anarejea katika shughuli zake.
 
Sabas alisema kwa mujibu wa maelezo ya Manga aliyeongea nao kwa njia ya simu alisema kuwa wakati anarudi nyumbani kwake Ngarenaro kulikuwa na gari aina ya Toyota Landcruiser Vx ambayo haikuitambua namba ilikuwa ikimfuatilia nyuma kwa muda mrefu.
 
Alisema mara baada ya kufunguliwa mlango wa geti wa nyumbani kwake watuhumiwa hao waliingia kupitia geti dogo lililokuwa wazi mpaka ndani na kuanza kumshambulia kwa risasi.
 
Kamanda Sabas alisema katika kujiokoa Manga alitoa bastola yake na kuanza kupambana nao kisha majambazi hao kukimbia wakimwacha akiwa amejeruhiwa kwenye mbavu.
 
Alisema Manga alikimbizwa katika hospitali ya Mkoa ya Mount Meru kwa ajili ya matibabu na aliruhusiwa usiku huo huo na kurudi nyumbani kwake kwa kuwa hali yake haikuwa mbaya sana.
 
‘’Manga amepigwa risasi ya kuparazwa ya ubavuni lakini hali yake inaendelea vema sana na yuko nyumbani kwake amepumzika”, alisema.
 
 Sabas alisema polisi inafanya uchunguzi wa tukio hilo ikiwa ni pamoja na kuwasaka wale wote waliohusika ili hatua za kisheria zichukuliwe dhidi yao.
 
Tukio hilo limeonesha kusikitisha baadhi ya wafanyabiashara wa madini Jijini Arusha na kusema kuwa polisi inapaswa kulifanyia kazi tukio hilo ili wahusika waweze kuchukuliwa hatua kali.

No comments: