RAIS Jakaya Kikwete amewashangaa wanasiasa wanaokosoa kitendo cha Serikali yake kukopa fedha nje ya nchi kuwa kinazidisha deni la taifa, kwamba hawana ufahamu na kufafanua kuwa katika kuharakisha maendeleo ya nchi, kukopa ni jambo la kawaida.
Alisema hata mataifa makubwa yaliyopiga hatua kubwa kwenye maendeleo
yamekuwa yanakopa na akasisitiza kuwa uamuzi wa serikali kwenda nje
kukopa amekuwa anaufanya ili kupata fedha kwa ajili ya kujenga
miundombinu ambayo itaifanya nchi ipige hatua kubwa kimaendeleo.
Alitoa mfano kuwa hata kama mtu anaeendesha duka ni lazima akakope
benki kama anataka kuendeleza duka lake, kama hatafanya hivyo kwa
kuamini kuwa fedha anazopata kwa kuuza bidhaa zitalitunisha duka hilo
basi asubiri miujiza ya kumpatia faida.
Aliyasema hayo wakati akizungumzia uamuzi wa serikali yake kuwenda
kukopa nje kwa ajili ya kujenga miundombinu mbalimbali, ikiwemo ujenzi
wa mkongo wa taifa ambao alisema lengo lake ni kuweka misingi ya
miundombinu wakati taifa linapoelekea kwenye utekelezaji wa ujenzi wa
viwanda vya kisasa.
Rais Kikwete alisema baada ya kufanya uamuzi huo aliamua pia kuwekeza
kwenye utafiti kwa kuhakikisha kuwa Serikal inatenga fedha kwa ajili ya
kuwasomesha watafiti, kununua vifaa vya utafiti na kukarabati vituo vya
utafiti ambayo alisema vingi vilikuwa kwenye hali mbaya.
“Tulianza na Sh bilioni 10, tunashukuru sasa hivi tupo kwenye Sh
bilioni 60 na naamini kuwa Rais atakayekuja ataendeleze juhudi hizi kwa
kutenga fedha zaidi kwa ajili ya tafiti maana nikiangalia hali ya
baadaye ya maendeleo ya nchi hii inategemea watafiti, wanasayansi na
wabunifu,” alisema Rais Kikwete.
Rais alisema anajivuna kwamba anaondoka madarakani wakati shughuli za
utafiti zimepata uhai na kwamba juhudi zilizofanywa na Serikali yake za
kuwaendeleza wabunifu zimezaa matunda mengi kwani kwa sasa nchi ina
watafiti wazee na vijana wanaofanya mambo makubwa yanayotambulika
kimataifa.
Alisema fedha zilizotolewa na serikali yake zimesaidia kusomesha
watafiti 517 katika kozi za shahada ya uzamili na uzamivu na vituo 20
vimekarabatiwa na miradi 70 ya utafiti imetekelezwa.
“Ndio maana nasema kiongozi anayekuja asipoliendeleza hili, mwambieni mzee unatuletea matatizo.”
Mkurugenzi Mkuu wa Costech, Dk Hassan Mshinda alisema kongamano hilo
la nne limewakusanya wanasayansi, watafiti, watunga sera na wabunifu
mbalimbali.
Alisema mada 80 zitajadiliwa ikiwemo tafiti mbalimbali zilizofanywa
na watafiti wa ndani, kujadiliana changamoto za kupeleka utafiti sokoni
na upatikanaji wa teknolojia na jinsi ya kuhuisha sayansi asili na
sayansi ya kisasa.
Dk Mshinda alimshukuru Rais Kikwete kwa kujali na kuwapa umuhimu
watafiti kuliko miaka ya nyuma na akasema kuwa anaamini kuwa msingi
uliowekwa utaendelezwa na awamu ijayo.
Alisema juhudi zilzofanyuwa na Rais Kikwete zimeungwa mkono na nchi
za Sweden na Finland ambao nao sasa wameamua kutoa fedha kusaidia juhudi
za serikali katika kufanya tafiti.
No comments:
Post a Comment