Serikali
imetoa mwezi mmoja kwa Mamlaka zinazohusika na masuala ya usalama
barabarani kuhakikisha zinakamilisha uboreshaji wa mfumo wa
kielektroniki wa uwekaji wa vifaa vya kufuatilia udhibiti mwendo
barabarani ikiwa lengo ni kushughulikia matatizo ya kiusalama barabarani
kupitia vyombo vya usafiri.
Akizungumza
hayo jijini Dar es Salaam, Naibu Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na
Mawasiliano Eng. Edwin Ngonyani amesema kuwa mfumo huo uendane na
utengenezaji wa mpango wa Taifa wa kufuatilia masuala ya kiusalama
barabarani utakaohusisha wataalam kutoka Jeshi la Polisi Kitengo cha
Usalama Barabarani, Mamlaka ya Udhibiti wa Usafiri wa Majini na Nchi
Kavu (SUMATRA) na Wataalam wa Idara ya Usalama na Mazingira (Sekta ya
Ujenzi).
"Shirikianeni
kutengeneza mfumo ambao utasaidia kutambua matatizo mbalimbali
yanayoweza kujitokeza barabarani ili kubaini mwenendo wa mabasi na
malori mwanzo hadi mwisho wa safari zake", amesema Naibu Waziri
Ngonyani.
Amesisitiza
kuwa mfumo ambao utaandaliwa na wataalam hao unatakiwa kukidhi mahitaji
ya kila mmoja ili kuleta matokeo chanya kwa manufaa ya nchi
yatakayosaidia kupunguza ajali za barabarani zinazotokana na mwendo
kasi, kupambana na uhalifu na kulinda usalama wa abiria.
Aidha,
Eng. Ngonyani amefafanua kuwa katika juhudi za kuhakikisha serikali
inapunguza ajali za barabarani wizara yake kupitia Idara ya Usalama na
Mazingira tayari imesaini mkataba wa kufunga kamera za udhibiti mwendo
kasi katika barabara kuu ya TANZAM (Dar es Salaam - Tunduma), ambapo
sehemu ya majaribio ya mradi huo imefanyika katika maeneo ya Dar es
Salaam - Chalinze - Morogoro.
Kwa
upande wake, Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Eng. Hamad
Masauni, amesema kuwa taratibu za kutengeneza mfumo huo zinatakiwa
kukamilika haraka ili kusaidia Jeshi la Polisi kutumia mfumo huo kuweza
kupambana na uhalifu katika maeneo mbalimbali ya nchi.
Ametanabaisha
kuwa Serikali itamchukulia hatua kali za kisheria mtu yeyote
atakaejaribu kuhujumu mfumo huo kwani serikali itatumia fedha nyingi
kuutekeleza kwa lengo la kuhakikisha usalama wa raia unalindwa ipasavyo.
Naye
Mkurugenzi Mkuu wa SUMATRA, Gilliard Ngewe, ameeleza manufaa ya mfumo
huo kwa wamiliki wa vyombo vya usafiri wa magari ya abiria na mizigo
kuwa ni itasaidia kupunguza matumizi ya mafuta, uharibifu wa matairi ya
magari mara kwa mara na kupunguza gharama za matengenezo ya magari.
Mfumo
huo wa kieletroniki wa usalama barabarani ni moja ya mbinu zinazotumiwa
na Serikali katika kuhakikisha matumizi ya usalama barabarani
yanazingatiwa kwa mujibu wa Sheria, Taratibu na Kanuni.
No comments:
Post a Comment