Monday, 21 August 2017

mashamba ya bangi ya ukubwa wa zaidi ya ekari 25 yateketezwa morogoro, watu watano watiwa mbaroni


Mkuu wa mkoa wa Morogoro, Dk Kebwe Stephen Kebwe (aliyeshika dumu) akimimina mafuta ili kuchoma lundo la bangi iliyokuwa imeng’olewa Augosti 19, 2017 na kikosi kazi maalumu katika moja ya mashamba ya bangi katika kitongoji cha Lufuna, Kijiji cha Masalawe, Kata ya Luale , Tarafa ya Mgeta, wilaya ya Mvomero .

Na John Nditi,  Morogoro

POLISI mkoani Morogoro kwa kushirikiana na Maofisa wa Mamlaka ya Kuthibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya nchini wamefanikiwa kuteketeza mashamba ya bangi ya ukubwa wa zaidi ya ekari 25 na kuwatia mbaroni watu watano akiwemo Mwenyekiti wa Kitongoji cha Lufuna , Asteri Telesphor (27). Watu hao miongoni mwao ni Mwenyekiti wa Kitongoji hicho baada ya kukutwa wakijihusisha  na  kilimo  bangi kwa njia ya umwagiliaji kando kando ya mto Mgeta, katika kijiji cha Masalawe, Kata ya Luale , wilayani Mvomero.

Operesheni hiyo maalumu ya kupambana na dawa za kulevya hasa kilimo cha bangi iliyofanyika  Augosti 19, mwaka huu   na kuongozwa Mwenyekiti wa Kamati ya Ulinzi na Usalama  mkoa , Mkuu wa mkoa wa Morogoro, Dk Kebwe Stephen Kebwe akiwa na  Maofisa wa mamlaka ya kuthibiti na kupambana na dawa za kulevya  pamoja na viongozi wa wilaya ya Mvomero.
Viongozi mbalimbali wa Vyombo vya Ulinzi na Usalama mkoa wa Morogoro na wilaya ya Mvomero walioongozwa na Mkuu wa mkoa Dk Kebwe Stephen Kebwe pamoja na askari Polisi wakiwa katika zoezi la kung’oa na kufyeka miche ya bangi kwenye moja ya mashamba ya bangi katika kitongoji cha Lufuna , Kijiji cha Masalawe, Kata ya Luale , Tarafa ya Mgeta, wilaya ya Mvomero .

Timu ya Opereshani hiyo ililazimika kuacha magari eneo la kijiji cha Homboza , Kata  Mlali  na kutembea kwa miguu kwa  muda wa zaidi  ya saa mbili kufika katika   vitongoji vya Lufuna na Tagata  vilivyopo kijiji cha Masalawe , kata ya Luale , Tarafa ya Mgeta , wilayani Mvomero  kwa ajili ya kutekeleza mashamba hayo. Kugundulika kwa mashamba hayo ni kufuatia   Vyombo vya Ulinzi na Usalama vya mkoa kupata  taarifa kutoka kwa wasiri juu ya uwepo wa uzalishaji mkubwa wa bangi eneo hilo.

Akizubngumza katika eneo la mashamba hayo , Kamishina wa Operesheni wa Mamlaka hiyo, Mihayo Msikhela alisema  , opereshani za kutekeleza dawa za kulevya hasa mashamba ya bangi  ni endelevu  kwenye maeneo mbalimbali nchini na kwa kushirikiana na vyombo vya Ulinzi na Usalama vya mikoa husika .

“ Serikali imekataza matumizi ya dawa za kulevya ikiwemo bangi na ili kutokomeza jambo hii opereshani za kushitumiza zitaendelea kufanyik maeneo mbalimbali nchini na kwamba serikali haijaribiwi” alisema Mihayo.
Mkuu wa mkoa wa Morogoro, Dk Kebwe Stephen Kebwe ( mbele ) akivuka mto Mgeta akifuatiwa na Kamishina wa Operesheni wa Mamlaka ya Kuthibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya nchini, Mihayo Msikhela , Aug 19, 2017 ili kushiriki na kikosi kazi maalumu kwa ajili ya kuteketeza shamba la bangi iliyolimwa kwa njia ya kilimo cha umwagiliaji kando kando mwa mto huo , katika kitongoji cha Lufuna , Kijiji cha Masalawe, Kata ya Luale , Tarafa ya Mgeta, wilaya ya Mvomero .

Naye  Kamanda wa Polisi wa mkoa wa Morogoro, Ulrich Matei alisema ,  watu watano walikamatwa katika opereshani hiyo akiwemo Mwenyekiti wa Kitongoji cha Lufuna , Kijiji cha Masalawe , Kata ya Luale Tarafa ya Mgeta , Asteri Telesphor (27) baada ya kukutwa  na kiroba cha bangi iliyoivuna kutoka shambani mwake.

Kamanda Matei aliwataja wengine waliokamatwa wanamiliki na kuhudumia mashamba hayo kwa njia ya kilimo cha umwagiliaji wa kisasa ni Pius Kalori  (35) maarufu kwa jina la Kikwili mkazi wa Kitongoji cha Tagata , Kalori Msimbe (50),Peter Kalori (27) na Justine Mathias wote wakiwa ni wakazi wa kitongoji hicho , Kijji cha Masalawe .

Katika opereshani hiyo ambayo ilidumu hadi alasiri  ya siku hiyo zaidi ya ekari 25 ya mshamba ya bangi ya watuhumiwa  hao  yaliyolima  kando kando mwa mto Mtega  kwenye  kitongoji hicho iling’olewa   na kutekelezwa kwa kuchomwa moto.
Moto ukiteketeza lundo la bangi iliyokuwa imeg’olewa Augosti 19,2017 na kikosi kazi maalumu kwenye moja ya mashamba ya bangi katika kitongoji cha Lufuna , Kijiji cha Masalawe, Kata ya Luale , Tarafa ya Mgeta, wilaya ya Mvomero .

Kwa upande wake, mkuu wa mkoa wa Morogoro, Dk Kebwe aliwataka wananchi wa eneo hilo na mengine kuacha kulima bangi na badala yake watumie fursa zilizopo katika uzalishaji wa mazao ya chakula na biashara ikiwemo maharage , mboga mboga  na kuutumia mto huo kwa kulima mazao halali na si bangi.

Mkuu wa mkoa  alisema , operesheni hizo zitakuwa endelevu katika ameneo mengine ya Wilaya ya Mvomero ambayo maeneo yake mengi ni vinara kwa kilimo cha bangi zikifuatiwa na wilaya ngingine kama Kilosa na Halmashauri ya wilaya ya Morogoro.

Wakizungumza wakiwa shambani mwao, watuhumiwa hao kwa nyakati tofauti walidai wamekua wakijihusisha na  kilimo cha bangi ili kupata fedha  za kujikwamua kiuchumi licha  ya matumizi ya bangi kukatazwa  kisheria.
Maofisa wa Vyombo vya Ulinzi na Usalama wa mkoa wa Morogoro pamoja na wilaya ya Mvomero wakiwa na askari Polisi wakivuka mto Mgeta , Aug 19, 2017ili kushiriki na baadhi ya wananachi wa Kitongoji cha Lufuna , Kijiji cha Masalawe , Kata ya Luale , Tarafa ya Mgeta ili kutekeleza bangi iliyokuwa katika shamba la kilimo cha umwagiliaji kando kando yam to huo.
Moja ya shamba la bangi la kilimo cha umwagiliaji iliyolimwa kando kando ya m to Mgeta katika kitongoji cha Lufuna , Kijiji cha Masalawe, Kata ya Luale , Tarafa ya Mgeta, wilaya ya Mvomero ambayo yalitekelezwa Augosti 19, 2017 na kikosi kazi maalumu cha kuthibiti na kupambana na dawa za kulevya.
Mkuu wa mkoa wa Morogoro, Dk Kebwe Stephen Kebwe ( wapili kulia ) akizungumza na askari wa kikosi kazi maalumu Augosti 19, 2017 baada ya kuteketeza mashamba ya bangi iliyolimwa kwa njia ya kilimo cha umwagiliaji kando kando mwa mto Mgeta , katika kitongoji cha Lufuna , Kijiji cha Masalawe, Kata ya Luale , Tarafa ya Mgeta, wilaya ya Mvomero . ( Picha zote na John Nditi).

No comments: