Mtakumbuka Serikali katika mwaka wa fedha uliomalizika 2016/2017 iliahidi kutoa Ajira serikalini zaidi ya 52,000 kwa
Watanzania, ambapo katika siku za hivi karibuni Serikali imekuwa ikitoa
vibali vya kuajiriwa watumishi wa kada mbalimbali ikiwemo Waalimu wa
Sayansi, Kada za Afya na maeneo mengine kulingana na mahitaji.
Kama mnavyofahamu mojawapo ya jukumu la msingi la kuanzishwa kwa
Sekretarieti ya Ajira katika Utumishi wa Umma ni pamoja na kuendesha
mchakato wa ajira kwa niaba ya waajiri mbalimbali na hatimae kuwapangia
vituo vya kazi waombaji kazi wanaofaulu usaili, ambapo tangu Serikali
ilipoanza kutoa vibali baada ya kusitishwa tumeshapokea jumla ya vibali
kwa ajili ya mamlaka za Ajira 239, kati ya hivyo vipo ambavyo vimeshafanyiwa kazi na vingine mchakato wake unaendelea katika hatua mbalimbali.
Aidha, baadhi ya vibali ambavyo mchakato wake umeshakamilika ni pamoja na kibali cha Mamlaka ya Chakula na Dawa (TFDA) ambayo tulipokea jumla ya maombi ya kazi 6,852 na walioitwa kwenye usaili kutokana na kukidhi vigezo walikuwa 2,949, kwa upande wa Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF) maombi yaliyopokelewa ni 9,022 na walioitwa kwenye usaili ni 1,550.
Aidha, miongoni mwa taasisi ambazo mchakato wake bado unaendelea ni pamoja na Chuo Kikuu cha Sayansi na Tiba Muhimbili (MUHAS) ambapo jumla ya maombi ya kazi 2,273 yamepokelewa na waliokidhi vigezo vya kuitwa kwenye usaili ni 144, maombi yaliyopokelewa kwa ajili ya Wakala wa Serikali Mtandao (e-GA),yalikuwa 5,732 na walioitwa kwenye usaili ni 4,054.
Taasisi nyingine ambayo mchakato wake unaendelea ni pamoja na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) ambayo ina nafasi wazi za kazi 400 na jumla ya maombi ya kazi 56,815 yamepokelewa
kupitia mfumo wa uwasilishaji wa maombi ya kazi kwa njia ya
kielektroniki “Recruitment Portal’ na baada ya kufanyiwa kazi waliokidhi
vigezo kwa mujibu wa sifa zilizokuwa zimeainishwa katika tangazo la
kazi husika na kuitwa kwenye usaili ni 29,674.
Pamoja na nia ya Serikali ya awamu ya tano kuendelea kuhakikisha
Watanzania wanaohitimu katika fani mbalimbali ndani na nje ya nchi
wanapata kazi, zipo changamoto kadhaa ambazo zimekuwa zikijitokeza
wakati wa utekelezaji wa mchakato wa ajira ambazo hupelekea baadhi ya
waombaji kazi kutoitwa kwenye usaili. Kama mlivyoona katika takwimu
zilizoainishwa hapo juu katika baadhi ya taasisi ambazo mchakato wake
umeshafanyiwa kazi kupitia Sekretarieti ya Ajira.
Aidha, tungependa mzifahamu changamoto hizo ili mtusaidie kuendelea
kuelimisha wadau wetu tukitambua mchango mkubwa wa vyombo vya habari
katika kuelimisha na kuhabarisha jamii ili nao waweze kuzifahamu,
kuzielewa na kuzifanyia kazi ili nafasi nyingine za kazi zitapotangazwa
waweze kuziepuka na kuwa katika nafasi nzuri na uhakika wa kuweza kuitwa
kwenye usaili na hatimae kupata kazi wanazoomba.
Changamoto hizo ni pamoja na Waombaji wengi kutokufahamu namna ya
kuandika barua za maombi ya kazi, kutoainisha nafasi wanazoomba,
kutokusaini barua za maombi ya kazi wanazoziwasilisha, kutokuthibitisha
nyaraka zao (certify) katika wanavyotakiwa
kufanya hivyo, hususan kwa waombaji waliosoma nje ya nchi kutowasilisha
vyeti vyao vya elimu kwa ajili ya uthibitisho wa kutambulika elimu
walizozipata katika mamlaka husika kama NECTA, NACTE na TCU kabla ya
kuzituma Sekretarieti ya Ajira.
Sambamba na hizo, ni baadhi ya waombaji kutokuambatisha nyaraka za
elimu hususani cheti cha kidato cha nne na sita au astashahada,
stashahada, shahada, shahada ya uzamili na kuendelea kulingana na elimu
waliyonayo.
Baadhi yao kutozingatia vigezo vya nafasi iliyotangazwa,
ikiwemo kudanganya sifa wakidai wamemaliza shahada ya fani fulani
ilihali hawajasoma shahada ya aina hiyo, au mwombaji mwenye elimu ya
astashahada kuomba kazi ya shahada, kuandika barua moja ya kuombea kazi
kwa nafasi tofauti, kutojua namna ya kuandika wasifu binafsi (CV),
waombaji wengi kuandika wadhamini wachache ambao ni ndugu zao badala ya
idadi ya wadhamini inayotakiwa ambao wanauwezo wa kutoa taarifa zao za
kitaaluma na kikazi kwa uhuru pindi wanapotakiwa kufanya hivyo.
Changamoto nyingine ni baadhi ya waombaji kazi wanapoelekezwa
kuwasilisha picha za utambulisho wao “Pasportsize” wao wanapakia kwenye
mfumo picha tofauti bila kujali mavazi wanayovaa, mandhari iliyotumika
na aina za picha wanazotuma.
Changamoto nyingine ni ya baadhi ya
waombaji kazi ambao ni Waajiriwa katika Utumishi wa Umma kutokupitisha
barua za maombi yao kwa Waajiri wao kabla ya kuziwasilisha Sekretarieti
ya Ajira, pamoja na baadhi ya waombaji kuja kwenye usaili wa mchujo au
mahojiano bila ya vyeti vyao halisi kama inavyoelekezwa.
Nyingine ni waombaji wengi kutozingatia masharti ya jumla ikiwemo,
kuwasilisha nyaraka pungufu mfano kutokuwasilisha barua ya maombi ya
kazi, kutokuambatisha baadhi ya vyeti vya taaluma, kuwasilisha maombi,
kwa njia tofauti na ile iliyoelekezwa kwenye tangazo la kazi,
kuwasilisha taarifa za uongo mfano, wasifu binafsi usio wa ukweli,
kutopakia taarifa sahihi (upload) katika maeneo husika ya mfumo wa
kuombea kazi pamoja na kupakia vyeti visivyokamilika mfano “result
slips, partial transcript, provisional result, progress report,
statement of result”.
Tumeainisha baadhi ya mapungufu hayo hapo juu ili wahitimu ambao ni
waajiriwa watarajiwa wafahamu hivi sasa soko la ajira ni la ushindani
mkubwa na linahitaji mwombaji aliyejiandaa vizuri.
Tunaamini endapo
muombaji yeyote wa kazi mwenye sifa na ambaye anazingatia maelekezo
yanayotolewa na Serikali kwenye maombi ya kazi anayowasilisha ataitwa
kwenye usaili. Kwakuwa wale ambao wahazingatii kikamilifu mara nyingi
hukosa fursa ya kuitwa katika usaili na kuikosa nafasi anayotarajia na
hatimae kusababisha malalamiko.
Aidha, ni vizuri wakafahamu Serikali inatumia gharama kubwa katika
kuendesha mchakato wa Ajira hadi kukamilika, na ni nia ya Serikali kuona
kila nafasi inayotangazwa inapata mwombaji makini mwenye sifa, ujuzi na
weledi wa kutosha kuweza kutumikia Taifa lake.
Mwisho, nimalizie kwa
kutoa rai kwa waombaji kazi wote wanaomba kazi serikalini kujiandaa
kikamilifu pamoja na kuzingatia masharti ya matangazo husika kwa
kuhakikisha wanaambatanisha nyaraka zinazotakiwa na kuomba nafasi za
kazi ambazo wana sifa stahiki.
Niwaahidi kuwa Sekretarieti ya Ajira
itaendelea kutoa elimu zaidi na kuwataka wale wenye changamoto ambazo
wanaona wanahitaji msaada wasisite kuwasiliana na taasisi kwa kufika
katika Ofisi za Sekretarieti ya Ajira au kupitia mawasiliano yetu katika
mitandao ya kijamii kama facebook.com/sekretarietiajira,
twitter.com/psrsajira, instagram:psrsajira au kwa simu za kiganjani
kupitia namba 0784398259/0687624975.
Imetolewa na; Kitengo cha Mawasiliano Serikalini, tarehe 24 AGOSTI, 2017.
No comments:
Post a Comment